EWURA walia kupotea maji, zao la mamlaka kutengua mwongozo wao

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:54 AM Apr 18 2024
KATIBU Mkuu wa Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa  Taarifa ya  Utendaji kazi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa Fedha 2022/23 iliyoandaliwa na EWURA, jijini Dodoma.
Picha: Maktaba
KATIBU Mkuu wa Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji kazi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa Fedha 2022/23 iliyoandaliwa na EWURA, jijini Dodoma.

MAJI ni uhai. Hilo linajulikana tangu historia ya uhuru wa nchi. Hadi sasa, msimamizi mkuu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), inaongozwa ya mwaka 2019.

Kitaifa na kimataifa, kuna malengo ya maendeleo endelevu kufika mwaka 2030, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, anasema uwezo wa miundombinu na uzalishaji maji umeimarika kwa asilimia 16.9, kutoka mita za ujazo milioni 744 hadi mita za ujazo milioni 870.

Andilile anasema, inaendana na kuongezeka uzalishaji maji kwa asilimia 1.8, kutoka mita za ujazo milioni 393 hadi mita milioni 400, huku wateja wa maji nao wakiongezeka kwa asilimia 11 kutoka, 1,385,485 hadi 1,532,362. 

Hata hivyo, anataja baadhi ya viashiria vya utendaji wa mamlaka za maji vimezorota, kama vile kupotea maji, ufanisi wa ukusanyaji mapato na kuzingatia ubora wa majitaka. 

MIONGOZO YA EWURA

Andilile, anafafanua kuwa mamlaka za maji zimeshafanyiwa tathmini kwa kuzingatia Mwongozo wa Vigezo vya Utendaji wa EWURA kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2022.

Anafafanua kuwa, kilichofanyika ni kuangalia utendaji wa jumla katika kutoaji huduma za majisafi na usafi wa mazingira wa mamlaka za maji; vilevile utendaji unaozingatia kutekeleza malengo ya katika mipango yao.

 Pia, anasema Mwongozo wa EWURA wa Kupunguza Upotevu wa Maji wa Mwaka 2021, umetumika kupima utendaji huo, ambao mamlaka za maji zinatakiwa kuhakikisha upotevu wa maji hauzidi asilimia 20 ya maji yanayozalishwa. 

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Kuchagua, Kufunga, Kupima na Kufanyia Matengenezo Dira za Maji kwa Mamlaka za Maji wa Mwaka 2021, mamlaka za maji zinatakiwa kuwa na sera, dira za maji na kanzidata, zitakazowasaidia kudhibiti upotevu wa maji.

MAJI YANAYOPOTEA

Ripoti hiyo, inaonyesha upotevu wa maji dhidi ya kiwango cha maji kinachozalishwa umeongezeka kutoka asilimia 35.5 mwaka 2021/2,2 hadi kufikia asilimia 37.2 mwaka 2022/23. 

Kiwango cha kupotea maji kinatajwa na ripoti kwamba, inachangiwa na utekelezaji dhaifu wa mikakati ya kupunguza kupotea maji. 

 Hapo mahsusi zinatajwa mamlaka maji 10 zenye kasoro kiasi ambazo ni: Kishapu, Maganzo, Busega, Nzega, Kashwasa, Mwanhuzi, Kasulu, Rujewa, Igunga na Kahama zilikuwa na upotevu wa maji chini ya asilimia 20. 

 Vilevile kuna zilizokuwapo katika hali mbaya na upungufu wa maji zaidi ya asilimia 50, ni mamlaka za maji 13, ambazo ni; Mahenge, Arusha, Mpanda, Vwawa-Mlowo, Makonde, Mpwapwa, Itumba-Isongole, Ifakara, Kiomboi, Rombo, HTM, Ushirombo na Mugango, pia Kiabakari. 

Katika mwaka wa fedha 2022/23, mamlaka za maji 17 kati ya 85, ambazo ni DAWASA, Kahama, Moshi, Musoma, Shinyanga, Tanga, Bukoba, Bariadi, Makonde, Maswa, Biharamulo, Bunda, Igunga, Ngara, Nzega, Utete na Busega zilikuwa na mkakati wa kupunguza upotevu wa maji.

  MATOKEO YA UDHIBITI 

Mkurugenzi – Andilile anasema matokeo yaliyopatikana kwenye sekta ya maji kutokana na udhibiti unaofanywa na EWURA kwa mamlaka za maji, ni pamoja na kupitia mipango iliyoandaliwa kwa kufuata mwongozo wa msimamizi huyo.

Hadi sasa, anazitaja mamlaka za maji zilizopunguza utegemezi serikalini, zikigharamia uendeshaji kwa kutumia mapato ya ndani na mikopo, kutekeleza miradi mikubwa, hata kufanikisha kuongezeka upatikanaji majisafi, pia kuhudumia majitaka.

“Mikataba hii umeimarisha utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira,” anasema 

Pia, anasema mfumo imara wa kutatua migogoro kati ya watoa huduma na wateja na uwapo wa miongozo na kanuni zinazofanya mamlaka za maji zifanye kazi kwa uwazi, zinaongeza uwajibikaji kwa mteja.

“Kuwapo utaratibu bora na wenye gharama ndogo za maunganisho mapya, kwa wateja na kupunguza muda wa mteja kusubiri maunganisho, baada ya maombi yake na kufanya malipo,” anasema Andilile.

Mkurugenzi huyo anasema, ni matokeo yanayotokana na ufuatiliaji wao, pia kuzijengea uwezo mamlaka za maji, ili kuhakikisha zinaandaa na kutekeleza mpango mkakati wa kupunguza maji yanayopotea nchini.

Hiyo inagusa katika maeneo ya sera za usimamizi wa dira za maji, mpango wa kufuatilia ubora wa majisafi na majitaka, pia mifumo ya utoaji taarifa za dharura kwa wadau na wananchi.

KATIBU MKUU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, anasema atazichukulia hatua mamlaka ambazo utendaji wake hauridhishi, kwa kuwa na kiwango kikubwa cha upotevu huo na kusuasua kwenye ukusanyaji wa mapato.

Anasema: “Hii haikubaliki hata kidogo. Sote tunajua kiwango cha upotevu wa maji kinachokubalika ni chini ya asilimia 20. Ni lazima mamlaka za maji ziweke na kutekeleza mikakati ya kuhakikisha zinapunguza kiwango cha upotevu wa maji.”

Anazitaka za maji nchini kuzingatia miongozo walinayo ya kudhibiti upotevu wa maji, kama vile ‘Mwongozo wa Kupunguza Upotevu wa Maji wa Mwaka 2021’ unaozitaka mamlaka za maji kuandaa mizani ya kupima viwango vya upotevu wa maji, kama zinavyoelekezwa  na Mwongozo wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wataalamu wa Maji (IWA).

Kuhusu ukusanyaji mapato,Mhandisi Mwajuma,  anasema ripoti inaonyesha kushuka kwa jumla ya mapato yaliyokusanywa kutokana na huduma ya majisafi na majitaka na shughuli nyingine za Mamlaka kwa takribani asilimia mbili, kutoka shilingi bilioni 401.48 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 393.34, mwaka 2022/23.

“Inatarajiwa kuwa uzalishaji unapoongezeka basi   na mapato yaongezeke. Mamlaka za maji ambazo zinajua zimezorota katika ukusanyaji wa mapato zijitafakari, sitakuwa tayari kufumbia macho watendaji wazembe,”anasema.