MKUTANO wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika 'Mission 300', unaomalizika Dar es Salaam wiki hii unafanyika wakati matarajio ya kuzalisha umeme katika Mradi wa Afrika wa Bwawa la Inga lililoko DRC yakiwa bado kitendawili.
Ukipewa jina la Grand Inga Project, ndani ya Mto Kongo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, unatajwa kuwa ni mradi mkubwa duniani wa kuzalisha umeme wa maji wa megawati 44,000.
Iwapo ungekamilika ungeweza kutosha kufikisha nishati hiyo sehemu kubwa ya Afrika Kusini ya Sahara. Unakadiriwa kuwa gharama yake ni karibu dola bilioni 80 takribani Sh. trilioni 20.
FAIDA
Kwa mujibu wa BBC, unakadiriwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa umeme wa maji duniani, wenye uwezo wa kuzalisha umeme mwingi zaidi kuliko Bwawa la Three Gorges la China.
Awali ulikuwa unafadhiliwa na Benki ya Dunia, ya Uwekezaji ya Ulaya na ya Maendeleo ya Afrika, ambazo zilihusika katika gharama za upembuzi yakinifu na tathmini za athari za mazingira, BBC inaongeza.
Hata hivyo kuna utata na kuna wasiwasi kuwa athari zinazoweza kujitokeza katika mazingira za mradi, ardhi, fidia na kama kuna manufaa yatapatikana kwa wawekezaji wa kigeni badala ya wakazi wa ndani.
Wakati mkutano wa 'Mission 300' ukiendelea kuandaa na kutoa Azimio la Nishati la Dar Es Salaam ni wazi kuwa kama mradi huo ungefanikiwa ungeweza kutoa msukumo mkubwa wa upatikanaji wa umeme kote Afrika na kuleta maendeleo hasa vijijini ambako huko ni giza.
Mkwamo wa Inga Dam, unaelezwa kuwa unatokana na kutokuelewana kuhusu uwazi kati ya serikali ya DRC na Benki ya Dunia mambo yanayochelewesha mradi huo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Lakini kikubwa ni kupata ufadhili unaohitajika wa dola bilioni 80, hasa wakati huu ambao mahitaji ya umeme ni makubwa lakini upatikanaji ni changamoto.
Mtandao wa International Energy Agency, unasema matumizi ya umeme yameongezeka walakini, Afrika bado ilikuwa na karibu watu milioni 600 wasio na umeme ni takwimu za 2020. Aidha karibu Waafrika bilioni moja hawana nishati safi ya kupikia.
Mtandao wa The Global Economy, unasema kuwa mahitaji ya umeme Afrika ni kilowati milioni 4.76 ili kuzilisha nchi 53 za bara hilo, utafiti wa mwaka 2022.
Hata hivyo kukwama kwa juhudi za Inga Dam si jambo la kukatisha tamaa kwa sababu Afrika ni tajiri namba moja wa vyanzo vya nishati duniani.
LIPO JUA
Afrika ina vyanzo vingi vya umeme kuanzia jua kali la mwaka mzima, makaa ya mawe, gesi asilia, maji, upepo, geothermal au joto ardhi na pia madini ya nyuklia.
Uhaba wa umeme Afrika ni jambo ambalo linahitaji wataalamu na viongozi wake kuliona kuwa halikubaliki kwa sababu kwanza uwepo wa wingi wa jua kali ni suluhisho.
Kwa mfano kugusa vyanzo vichache kama jua na makaa ya mawe kunaweza kuleta mafanikio makubwa wakati Inga inakwama.
Ikumbukwe ni bara linalowaka jua mwaka mzima inakuwaje lisitumie sola au nishati jua?
Januari hii jua ni kali kote Afrika maeneo mengi yana viwango vya juu sana vya mwanga wa juakali na mionzi ya ‘Ultra Violet’ ni mingi ikichangia kuleta athari. Kuna karibu saa saba mpaka tisa za siku yenye jua kali likichoma Waafrika.
Kutokana na Afrika kuwa mojawapo ya mabara yenye jua huku sehemu kubwa ikipokea viwango vya juu vya mionzi ya jua, kiwe chanzo kikuu kitumiwe.
Uwepo wa jua kali mwaka mzima uwe kichocheo cha kuwa na umeme wa kutosha, Mission 300 ianze na jua kuongeza ubunifu na ugunduzi ili watu milioni 600 wanufaike na chanzo hicho ambacho kimejaa kila kona.
Tanzania, Uganda, Misri, Chad, Niger, Sudan, Sudan Kusini, Kenya na Madagascar kwa ujumla ukanda mzima wa Sahel na Sahara umejaa jua na huo uwe mkakati wa Afrika wa kuwa na umeme wa uhakika badala ya kujiingiza kwenye miradi ya gharama kubwa inayoongeza deni lake kutoka taasisi za fedha.
Lakini wakati tunatarajia kusoma Azimio la Nishati la Dar es Salaam litakalotolewa na ‘Mission 300’ Afrika isiache kutumia vyanzo vyote vya nishati ambavyo vilileta mapinduzi ya viwanda na maendeleo katika nchi tajiri na zilizoendelea.
Afrika iwekeze kwenye utaalamu, ubunifu na mbinu za kisasa kutumia madini ya urani kuzalisha umeme. Mbona Marekani na nchi nyingine zinatumia vinu vya urani kuzalisha umeme, Afrika inakwama wapi?
Taarifa za kimtandao zinaeleza kuwa Marekani inatumia umeme wa nyuklia, ikizalisha karibu asilimia 20 ya umeme wa nchi hiyo na kuifanya kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa nishati ya nyuklia duniani, Afrika kwanini ishindwe? Wataalamu wapo watumike kufikia azma hiyo.
Afrika ishirikiane kutumia rasilimali zake kuzalisha umeme, mathalani Tanzania ina makaa ya mawe tani takribani tani bilioni 1.5.
Madini hayo yako Ngaka mkoani Ruvuma, kuna Mchuchuma wilayani Ludewa na Kiwira kama kuna tani zaidi ya bilioni 1.5 kwanini Tanzania isiwe kitovu cha kuzalisha umeme wa makaa ya mawe Ukanda wa Kusini mwa Afrika?
Inakuwaje Zambia inasafirisha shaba ghafi kwa miaka 60 wakati kuna makaa ya mawe yanayoweza kuzalisha umeme na kuiyeyusha, kuichakata na kuiongezea thamani ili kupata faida zaidi?
Hata sasa kwanini Tanzania iendelee kuagiza chuma nje wakati kuna hifadhi ya chuma cha kutosha Liganga?
Kinachohitajika sasa ni kanda za kiuchumi kama SADC, COMESA na EAC, kuungana na kuanzisha miradi ya kuzalisha umeme mfano wa makaa ya mawe ili chuma kutoka Mchuchuma na Shaba ya Zambia ziyeyushwe na kuuzwa zikiwa na thamani zaidi.
Pia vyuma (ingots) vitumiwe kuunda bidhaa kama mabati, magari, reli na meli hapa Afrika hata kuuzwa nje kwa faida.
Pamoja na kuwa na viwanda mradi huo uchangie kuwa na nishati kwenye gridi ya Afrika huku ukifua madini kama chuma na shaba na kusongesha mbele uchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED