CHADEMA inavyopigilia msumari ‘no reforms no election’

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 09:29 AM Feb 05 2025
Tundu Lissu Mwenyekiti Taifa  CHADEMA, anayechaguliwa mwaka huu
Picha: Mtandao
Tundu Lissu Mwenyekiti Taifa CHADEMA, anayechaguliwa mwaka huu

BAADA ya CHADEMA kumaliza uchaguzi na kusimika viongozi wapya, inageukia ajenda ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ikisema ‘no reforms no election’, kumaanisha bila mabadiliko hakuna uchaguzi.

Tundu Lissu Mwenyekiti Taifa CHADEMA, anasisitiza msimamo huo huku akisema muda uliopo unatosha kufanya mabadiliko wanayohitaji.

Lissu anasisitiza msimamo huo alipokabidhiwa rasmi uongozi wa chama hicho kwenye  makao makuu Mikocheni jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Katika hotuba yake, anafafanua kwamba kuna uchaguzi mkuu Oktoba na kuna ‘no reforms no election’ hayo mambo mawili hayaendi pamoja na tafsiri yake kama hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi, si kwamba watasusia haki hiyo ya kidemokrasia.

 “Sitaki nizungumze hapa zaidi tunaenda kujifungia tutaamua hautakuwa uamuzi wangu, bali wa chama, tutakaa na viongozi tutatoa  msimamo,” anasema akikaribishwa kwa kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho waliofika kumkaribisha ofisini.  

Anasema wanapaswa kuzungumza lugha pekee anayoweza kuielewa Rais Samia Suluhu Hassan na wataizungumza kwa nguvu kwa sababu hakuna yeyote anayetaka uchaguzi uwe kama wa mwaka 2020.

 “Tutaonana na marafiki zetu duniani tuwaambie msimamo wetu hadharani tutawaomba watuunge mkono, na wale wasiotupenda tutawaangalia usoni kuwaambia msimamo wetu ni huu,” anasema Lissu mwanasheria mbobezi.

Anatangaza kuwathibitishia wanaosema uongozi mpya ni wa wabangaziaji kwa kufanya kazi na kuleta mabadiliko ndani na nje ya chama.

Anapoulizwa kama msimamo huo utafanikiwa na kipi kipya kinachowapa ujasiri, anasema suala hilo linakwenda kutengenezewa mkakati na kamati kuu ilitoa azimio na mkutano mkuu umelikubali.

Anasisitiza msimamo huo wa ‘no reforms na election’ siyo wake bali ni wa chama na kwamba kazi yake ni kutekeleza maagizo ya CHADEMA.

Hata hivyo anasema hiyo haina maana hana mawazo yake juu ya msimamo huo, akitoa ufafanuzi zaidi. 

Anaanza kuwahoji wafuasi wake “Mahali tulipo nani anaweza kasema tukienda kwenye uchaguzi ujao kwa sheria na tume iliyopo watapata chochote? Anyooshe mkono.

Wafuasi hao kwa sauti moja wanajibu “haiwezekani” hapo akasisitiza tukisema twende katika uchaguzi wao wanajua na Mungu anajua tunaenda kudhulumiwa na wengine kuumizwa.

Anasisitiza katika mazingira hayo, hawawezi kwenda kunyolewa tena na kwamba hawatokuwa kama kondoo anapelekwa kila siku machinjioni akiwa amenyamaza.

“Ninaamini na nina ushahidi wa kutosha wa chaguzi tatu, wapo wanaounga mkono ninachokiamini ‘no reform no election’ tunazungumzia njia zisizo za kawaida za kufanya siasa, tunazungumzia kushurutisha mageuzi, kupata mageuzi kwa shuruti kama walivyopata Kenya, Malawi, bunge linaweza likakaa muda wowote hata bila kuwa na ratiba,” anasema Lissu. 

Katika kutetea hoja yake, anakumbusha kuwa bunge liliwahi kuitishwa kwa dharua Jumamosi ukumbini Karimjee kuidhinisha hoja ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hata leo upo.

“Katiba inasema bunge likivunjwa linaweza kuitishwa muda wowote kabla ya uchaguzi mkuu, na sisi tutanyamaza tukiwa tumekufa hata tukiwa gerezani tutapambana kutoka gerezani,” anasema Lissu.

Anaeleza kuwa wakifanya harakati sawasawa anaamini mageuzi yatatokea na uchagzui utafanywa kukiwa na mfumo mpya.

Vilevile Lissu anawakaribisha watu wanotaka kujiunga na chama hicho akisema milango ipo wazi akisisitiza chama hicho kinahitaji jeshi kubwa na karama.

WASIRA AGUSWA

Makamu Mwenyekiti CHADEMA, John Heche, anatuma ujumbe kwa  Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Stephen Wasira kwamba umri umesonga na hana jipya.

“Nimemuona mzee Wasira amekuwa serikalini kwa miaka 80 anataka atengeneze kama anashindana na mwenyekiti wetu Lissu, Wasira, Lissu si saizi yako, huyu anapambana na Rais Samia Suluhu Hassan si wewe.

“Hatuna nafasi ya Lissu kushughulika na wewe mmekuwa serikalini kwenye nchi iliyojaliwa rasilimali za kutosha lakini Watanzania wamebaki masikini kwasababu ya mawazo ni yaleyale yaliyoshindwa.”

Anadai wanafanya mabadiliko kwa viongozi wale wale Wasira ni yuleyule, hawezi kuleta mabadiliko, ameshiba kwa sababu analipwa mshahara tangu akiwa na miaka 20 mapaka leo akiwa na miaka 80 na hajui vijana wanavyotaabika.

Anaongeza kuwa ni shibe hiyo, ndiyo maana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alimjibu ovyo mjamzito aliyepiga simu akilalamikia kukosa huduma za uzazi katika hospitali ya umma.

“Mgonjwa alimpigia simu kumwambia hana ‘gloves’ akamjibu amwambie mume wake achukue mkasi amzalishe hebu fikiria kiwango hicho cha uongozi kwa hali hiyo. Hawa ni watu waliojisahau kwa kiwango kikubwa,” anasema Heche.

Anaongeza kuwa  kutokana na hali hiyo, CHADEMA itawakumbusha wajibu wao na itawaondoa madarakani, akikumbushia kuwa Chalamila ni mteule wa Rais maana yake alichosema ni kauli yake.

Anatamba CHADEMA inarejea kufanya kazi yake, huku akilihadharisha Jeshi la Polisi kuwatisha kwa kuwa ni chama kilichosajiliwa kisheria.

Anasema hakuna mwanachama atakayepata upendeleo katika nafasi fulani kwa sababu alimuunga mkono Lissu au yeye na hivyo uwezo ndio utamweka katika nafasi ya uongozi.

Chama hicho, kimekuwa imara na kitaendelea kubaki imara huku akiwataka wafuasi wake kuondoa shaka kuwa kitakufa.

KUANDAA MKAKATI

Katibu Mkuu John Mnyika anasema CHADEMA na viongozi wapya na wastaafu watajifungia ndani kwa wiki moja kuandaa mkakati wa pamoja kuelekea uchaguzi mkuu.

"Uongozi huu ni wa awamu ya saba ni mpya lazima tupate wasaa kukaa kupanga mipango kesho tutajifungia viongozi wakuu wote wastaafu kwa pamoja tutatoka na mwelekeo mpya tutaanza kuzunguka kuendesha mapambano katika taifa letu."

Kuhusu mkutano wake kuzuiwa na Jeshi la Polisi siku chache zilizopita anasema, alitaka kueleza mambo ya kuyapatia kipaumbele na ujio wa mwenyekiti wa katika ofisi za chama.

Aidha, anatumia mkutano huo kulaani kitendo cha jeshi hilo kuzuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuwa sheria inawaruhusu.

 “Polisi waliweka ‘difenda’ karibu na geti la kuingilia wakaanza kuwazuia waandishi wa habari kufanya kazi yao wakati hata katikati ya vita wanaruhusiwa kutimiza majukumu yao.

Anasema watajifungia kuanzia viongozi wote na wastaafu kwa ajili ya kupanga mipango kwa pamoja kutoka na mwelekeo mpya, baada ya hapo wataanza kuzunguka kuendesha mapambano katika taifa.

Anawataka wana-CHADEMA kuachana na tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi na baadala yake wasonge mbele kwa nguvu ya pamoja kufanikisha agenda ya mageuzi.

Kuhusu aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutoonekana wakati wa makabidhiano ya ofisi anasema katiba ya chama chao inaruhusu Katibu Mkuu kusimamia na kwamba hakuna shida kama watu wanavyodhani.

Chama hicho kimefanya uchaguzi kwa kumchagua Lissu kuwa Mwenyekiti Taifa ambaye awali alikuwa Makamu akichuana na aliyekuwa Mwenyekiti Mbowe.

Ni uchaguzi ambao wajumbe walikesha kusubiri hatima, Lissu akiibuka mshindi kwa tofauti ya kura 31.