MAENDELEO ni lazima, lakini yasipogusa maisha ya watu hayana maana, ni sharti yawaguse wananchi na kubadilisha maisha yao.
Kuboresha maisha ya watu ni pamoja na kuwapa elimu bora, huduma bora za afya, maji, umeme, barabara, masoko, ajira, uwekezaji na uhakika wa chakula ili kumgusa kila mmoja na asiachwe hata mmoja.
Kimsingi, serikali inawajibika moja kwa moja kwa wananchi kwa kuwapatia maendeleo kupitia kupanga na kutekeleza miradi kwa mujibu wa dira, vipaumbele, miradi ya kimkakati na kwa maelekezo ya katiba ili kufikia ustawi wa maisha ya raia.
Miongoni mwa jambo ambalo limepewa msukumo mkubwa na serikali ya awamu ya sita ni ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi – PPP. Kuanzia 2022, Rais Samia Suluhu Hassna, anamteua David Kafulila kuwa kamishna wa PPP ili kuwe na msukumo wa kipekee katika ushirikiano wa maeneo hayo kwa lengo la kufikia ustawi wa wananchi.
Ni ukweli kuwa ujenzi wa taifa unahitaji juhudi za pamoja. Wakati mwingine baadhi ya wananchi wamekuwa na dhana potofu kuwa serikali peke ndiyo yenye wajibu wa kufanya kila kitu bila kujua kuwa hata mtu binafsi, kampuni na AZAKI ni sehemu ya ujenzi wa nchi.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa miradi ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi inaibuliwa ili kutatua kero za wananchi badala ya kutegemea na kusubiria fedha kutoka serikalini pekee kuboresha maisha ya Watanzania.
Sekta binafsi ni mdau muhimu wa maendeleo na pale inapokuwa imara mchango wake unakuwa mkubwa na hivyo maisha ya wananchi wanakuwa bora zaidi. Ndiyo maana zama hizi kunahitajika uzoefu, utaalamu na raslimali fedha za kutosha katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Hivi karibuni Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dodoma kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia wa Sekta za Umma na Binafsi (PPP) wameshirikiana ili kufanikisha azma ya kujenga mabweni ya wanafunzi kwa ubia yakigharimu Shilingi bilioni 20.7.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha CBE, Prof. Edda Lwoga, ubia huo unatokana na changamoto ya mabweni katika kampasi kuu ya jijini Dar es Salaam na kwamba chuo kina wanafunzi 12,000 lakini mabweni yaliyopo ni mawili yenye uwezo wa kuchukua vitanda 160 pekee vya wanafunzi wa kike na kiume.
Vitanda hivi 160 ni sawa na asilimia 1.34 huku kukiwa na upungufu wa vitanda kwa asilimia 98.6, anaongea Profesa Lwoga.
“Mradi huo utafanywa kwa ubia kati ya CBE na mwekezaji lakini pia naomba nitumie nafasi kuwafahamisha wadau, wawekezaji wa ndani na nje kuhusu fursa hii muhimu ya uwekezaji ili waweze kushiriki kwenye mkutano maalumu utakaokutanisha wadau mbalimbali katika kuupelekea mradi huu sokoni na kupeana uelewa zaidi…,” anasema Profesa Edda.
Ubia kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu kutokana na uwepo wa changamoto katika sekta ya elimu kama vile upungufu wa madarasa, madawati, meza, viti na samani nyingine, mabweni, mabwalo, nyumba za walimu, kumbi za shule, mafunzo kazini kwa walimu na vifaa vya TEHAMA. Nguvu ya pamoja baina ya sekta hizi mbili inachagiza utatuzi wa changamoto katika sekta ya elimu.
Uhitaji mkubwa wa mabweni katika chuo cha CBE utapungua kutoka asilimia 1.34 iliyopo sasa hadi asilimia 30 mradi huo wa ujenzi wa mabweni utakapokamilika.
“Hali iliyopo imesababisha uhitaji mkubwa wa malazi ya wanafunzi kwa asilimia 98.6 hivyo wengi wanalazimika kutafuta malazi nje ya chuo kwa gharama kubwa, jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu. Njia ya PPP ni bora na ya haraka kufanikisha mradi huu, ambayo itawanufaisha wanafunzi.
CBE imejikita katika kutoa mazingira bora ya kujifunzia na kuboresha malazi ya wanafunzi ni kipaumbele muhimu kwetu nawashukuru washirika wa sekta binafsi, serikali na wadau wote kwa mchango wao katika kufanikisha mradi huu muhimu, anasema Prof. Edda.
Mwezi uliopita Kamishna wa PPP, Dk. Kafulila, anausifu ubunifu uliofanywa na CBE katika kutatua changamoto ya mabweni, na hivyo kutoa wito kwa vyuo vingine kuihusisha sekta binafsi katika ujenzi wa mabweni na miradi mingine ya maendeleo.
“Kila mradi ambao sekta binafsi inaweza kuutekeleza kwa teknolojia ya hali ya juu kuliko serikali basi ipewe nafasi ili tujenge uchumi wa kisasa ambao sekta binafsi ndiyo ina nafasi kubwa ya kutengeneza ajira nyingi. Utaratibu wa ubia unaleta unafuu kwa serikali kwa sababu miradi inajengwa bila kutegemea fedha zake lakini utaratibu huu wa ubia unafanya serikali ivute teknolojia ya kujenga baadhi ya miradi, teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa inapatikana sekta binafsi,” anasema Kafulila.
Sekta binafsi ina nguvu ya fedha, ujuzi, uzoefu na teknolojia katika kumudu majukumu ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu. Kwahiyo, ni muhimu kwa viongozi serikalini kuishirikisha ipasavyo katika miradi mbalimbali ya elimu ili kuboresha sekta ya elimu.
Sanjari na hilo, ni muhimu kuzingatia kuwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi si ubinafsishaji, unaolenga kuunganisha nguvu ya pamoja, miradi ya ubia inabaki kuwa mali ya serikali, huku sekta binafsi ikiwa mshirika muhimu, na baada ya kurejesha gharama zake za uwekezaji kwa mujibu wa mikataba, serikali ni mmiliki kwa asilimia 100.
Ni vyema sekta binafsi ikapewa ushirikiano badala ya kuwekewa vigingi katika kuboresha elimu kwani ni wadau muhimu kwa maendeleo. Naamini miradi ya ubia katika eneo hilo ni muhimu kuanzia elimu ya awali, sekondari, vyuo vya kati hadi juu.
Mwandishi ni Mwalimu wa Sekondari ya Mlali mkoani Dodoma.
Maoni: 0620 800 462
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED