MIONGO MITATU; Goma, kitovu cha mgogoro Mashariki mwa DRC

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 02:13 PM Jan 28 2025
Baadhi ya wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakilinda doria Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
Picha: DW
Baadhi ya wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakilinda doria Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

KWA miongo mitatu huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), hali si shwari

Maelfu ya wakazi wa eneo hilo wameathiriwa ikiwamo vifo, njaa, makazi , afya na elimu. 

Japo eneo hilo linalojumuisha majimbo ya Ituri, Kivu kusini na Kivu Kaskazini, yana jumla ya makundi ya wapiganaji zaidi ya 129, kundi la waasi la M23, ambalo ndilo kuu lililobuniwa baada ya makubaliano ya kutafuta amani imekuwa na historia ya machafuko.

Mji wa Goma umekuwa kitovu cha mzozo wa kikanda uliodumu kwa miongo kadhaa. Mapigano kati ya kundi lenye silaha linalojulikana kwa jina la M23 na jeshi la DRC, yamezidi katika eneo hilo na kuwafukuza zaidi ya watu 400,000 kutoka makwa

Wakazi wakiyahama maeneo yao
KUNDI LA M23 LINA NGUVU GANI

Kundi la M23, ni kundi lenye silaha ambalo lilijitenga na jeshi la DCR, miaka 10 iliyopita kwa madai ya kuwalinda Watutsi ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi. 

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN), wanasema kuwa, kundi hilo linaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, ambayo pia inaongozwa na Watutsi, jambo ambalo serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha mara kwa mara. Kwa mujibu wa BBC.

Rwanda imesema hapo awali kwamba mamlaka nchini DR Congo, inashirikiana na baadhi ya waliohusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Mwaka 2012, waasi waliikalia Goma kwa siku 10, kabla ya kuiacha kufuatia shinikizo la kimataifa.

Lakini, mwaka 2021, kundi hilo lilichukua tena silaha, likisema ahadi zilikuwa hazijatimizwa.

M23 tangu wakati huo, wamechukua udhibiti wa maeneo mengi zaidi katika eneo la mashariki kuliko hapo awali. 

Wataalamu wa UN wanasema, Rwanda ina hadi wanajeshi 4,000 wanaofanya kazi pamoja na M23 mashariki mwa DRC.

ILIKO GOMA

Iko eneo la ufuo wa kaskazini mwa Ziwa Kivu, kwenye mpaka wa Rwanda. Goma daima imekuwa kitovu muhimu cha kisiasa na kibiashara.

Mji huo, una watu zaidi ya milioni moja na kuufanya kuwa moja ya miji yenye watu wengi zaidi DRC. 

Kutokana na udongo wake wa volkano, wenye rutuba, kihistoria mji huo umekuwa kituo cha biashara chenye shughuli nyingi na nchi jirani ya Rwanda.

Goma, ni mojawapo ya miji mikuu ya uchimbaji madini inayosambaza madini yanayohitajika sana kimataifa kama vile dhahabu, bati, kobalti na koltani.

Ina barabara muhimu za kimkakati za usafiri wa barabarani na angani. 

Pia ina kambi kubwa ya walinda amani wa UN, suala ambalo limevutia biashara nyingi, mashirika ya kimataifa na balozi.

UTAJIRI WA GOMA

DRC, inakadiriwa kumiliki asilimia 70 ya madini ya kobalti duniani. Ni madini muhimu katika kuwezesha betri za lithiamu-ion katika simu za mkononi, magari ya umeme na aina nyingi za sigara za kielektroniki.

Huku dunia inapojitolea kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kuhama kutoka kwa nishati ya kisukuku, kuna ongezeko la mahitaji ya vyanzo safi vya nishati.

Tishio la vita vipya vya DRC, linaweza kuvuruga ugavi wa kimataifa, kupanda kwa bei na kusababisha uhaba katika tasnia ya teknolojia na nishati safi.

MAMLAKA

Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, mwaka 2023 alisema kuwa Goma, haitatekwa kamwe. 

Ahadi zake za kuhakikisha kuwa mji huo hauna waasi zilikuwa juu kwenye orodha yake ya ahadi kwa watu wa DRC, ikimaanisha kutekwa kwa Goma kungemuathiri kisiasa kiongozi huyo aliyechaguliwa tena.

DRC, imekata uhusiano wote na nchi jirani ya Rwanda, jambo ambalo limesababisha onyo kutoka kwa Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres kwamba mzozo wa sasa unaweza kuhatarisha kuongezeka kwa vita vya kikanda.

Kuongezeka kwa mzozo kunaweza pia kusababisha uhaba wa rasilimali za kibinadamu, ambazo tayari zimepungua kutokana na machafuko mengine.

Wakati M23 inasonga mbele katika eneo la mashariki, maelfu katika vijiji vidogo wanayahama makazi yao na kuelekea katika hospitali za karibu huko Goma, jambo ambalo linawalemea.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limeonya juu ya kuongezeka kwa hatari kwa raia, huku jeshi la DRC likipambana na waasi wa M23. 

Wakazi wengi wamehama makazi huko Goma
Kundi la misaada ya kibinadamu linashutumu pande zote mbili, kwa kutekeleza unyanyasaji mkubwa dhidi ya raia.

Mamlaka ya DRC inasema vikosi vya serikali na washirika wao wanaopigana katika eneo la Mashariki ya nchi hiyo, bado wana udhibiti wa baadhi ya maeneo huko Goma, licha ya kuingia kwa M23 jijini siku ya Jumatatu.

Rais Tshisekedi alifanya mkutano na viongozi wa taasisi kadhaa za serikali mwishoni mwa Jumatatu, jana, ili kutathmini hali ilivyo huko Goma, mji mkuu wa Mkoa wa Kivu Kaskazini ambao kikundi cha M23 kinadai kuwa imeuteka.

Chanzo: BBC/DW