JESHI la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya mama Mwamvita Mwakibasi (33) na mtoto wake Salma Ramadhan (12) nyumbani kwao, eneo la Mkonze, jijini Dodoma.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Alchelaus Mutalemwa aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Daudi Nyakungo (45), Rajab Rashid (45) na Fikiri Steven (40), wote wakazi wa Mkonze wanaohojiwa na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Kaimu Kamanda Mutalemwa alisema kuwa watu hao waliokuwa wakazi wa Mkonze, mtoto alikuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mkonze, walifariki dunia wakiwa wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.
"Walipigwa kitu butu kichwani wakiwa wamelala nyumbani kwao na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji saa nane usiku Septemba 6, 2024," alisema.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, pia kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Juzi, miili yao wanafamilia hao ilisafirishwa kwenda Kiteto, mkoani Manyara kwa ajili ya maziko.
Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo, Diwani wa Mkonze, David Bochela aliwaomba wananchi wote kuwa watulivu na kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha mitaa yao inakuwa na usalama.
Mchungaji wa Kanisa la Assembly of God katika Mtaa wa Mkonze, Festo Mahinyila alitoa rai kwa serikali kuangalia kwa jicho la tatu nini kinaendelea katika jamii na sababu yake nini.
"Kwa upande wetu kama viongozi wa dini, tuchukue hatua ya kumrudia Mungu na kuwaita watu kumrudia Mungu, tufanye makongamano ya maombi ya kuomba toba na rehema kwa Mungu kwa kuwa ni vitendo ambavyo vinamchukiza Mungu wa mbinguni," alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu nchini (Bakwata), Shekhe wa Kata ya Mkonze, Jumanne Kisaka, alisema tukio hilo linaonesha kukosa hofu ya Mungu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED