Watoto wadaiwa kuua mzazi kikongwe, miaka 103

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:06 PM Feb 25 2025
ma
AI
ma

JESHI la Polisi Mkoa wa Geita, linawashikilia watu watatu wa familia moja kwa tuhuma ya mauaji ya baba yao mzazi Hussein Bundala, mwenye umri wa miaka 103.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo amebainisha hayo Februari 24, mwaka huu, wakati akizungumza na vyombo vya habari mkoani hapo.

Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo
Waliokamatwa ni Yombo Hussein Bundala(75), Makame Hussein Bundala (53) na Shija Hussein Bundala (50) na kuwa watu hao wanadaiwa kutekeleza mauaji hayo Februari 5, 2025 majira ya usiku katika kitongoji cha Ihanamilo, Kata ya Nyamtukuza wilayani Nyanghwale, mkoani humo.

Aidha amesema uchunguzi wa awali unaonesha marehemu aliuwawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwani, usoni na shingoni.

“Jeshi la polisi linaendelea kukamilisha uchunguzi wa tukio hili kwa kushirikiana na taasisi nyingine za ulinzi na usalama ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo,” amesema Jongo.