Watanzania 80% kufikiwa nishati safi

By Allan Isack , Nipashe
Published at 10:03 AM Sep 03 2024
Makamu wa Rais, Dk.  Philip Mpango (katikati), akishiriki katika Ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
PICHA: OFISI YA MAKAMU WA RAIS
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango (katikati), akishiriki katika Ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema serikali imejipanga hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania, watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia nyumbani ili kuepuka ukataji wa miti unaochangia uharibifu wa mazingira.

Aidha, amesema uchafuzi wa mazingira ndani ya nyumba unaotokana na kupikia kwa kuni na mkaa ni miongoni mwa sababu kuu zinazoharibu mazingira na kuleta matatizo ya kiafya.

Dk. Mpango alisema hayo jana jijini hapa wakati akifungua Jukwaa la 24 na Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), ambao nchi ya Tanzania imekuwa mwenyeji.

Alisema Tanzania imekuwa kinara kwa bara la Afrika kwa ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nyumbani (AWCCSP), kupitia Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa bingwa wa kipaumbele cha kusimamia ajenda hiyo.

Pia, lengo la kutumia teknolojia hiyo ni kuwaondolea mzigo wanawake kutumia mkaa na kuni kupikia.

“Kwa ushirikiano na washirika wetu wa maendeleo, jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 2.2 zilikusanywa katika Kongamano la Nishati Safi ya Kupika huko Paris, Mei 2024, haya ni maendeleo ya kutia moyo ambayo yatasaidia kukabiliana na changamoto za kimazingira, kiafya na kijamii na kiuchumi zinazohusiana na matumizi ya nishati asilia ya kupikia,” alisema Dk. Mpango.

Kadhalika, serikali imejipanga ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, kutoka asilimia saba ya sasa.

Alisema Tanzania inakabiliwa na athari kadhaa za mabadiliko ya hali ya hewa ya ukubwa usio na kifani, ikiwamo Desemba 2023, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara.

Watu 89 walifariki dunia, 139 walijeruhiwa, zaidi ya watu 1,500 waliathirika na nyumba 95 zikisombwa na maji.

Aidha, kulikuwa na uharibifu katika miundombinu na serikali ililazimika kuwahamisha watu na kutumia takriban Dola za Kimarekani milioni tatu kukarabati na kujenga nyumba na barabara mpya katika eneo hilo lililoathirika. 

Alisema uharibifu wa mtandao mzima wa barabara za kitaifa ulikuwa kilomita 520, ambazo zitahitaji Dola za Kimarekani milioni 355 kukarabati na ujenzi mpya, ustahimilivu wa hali ya hewa sasa umekuwa mojawapo ya viashiria muhimu na kanuni za msingi za ugawaji wa rasilimali za bajeti kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025.

“Mabadiliko ya hali ya hewa na ukosefu wa usawa wa kijinsia ni changamoto, lakini Tanzania imeendelea kuhimiza ujumuishaji wa masuala ya jinsia na mabadiliko ya tabianchi katika sera, programu na mikakati katika ngazi zote kwa kuweka vipengele muhimu vya sera za usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa fursa za kiuchumi na kifedha kwa wanawake na wanaume kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika ngazi zote za uongozi na maamuzi,” alisema.

Mabadiliko ya hali ya hewa yameleta athari katika mifumo ya ikolojia, usalama wa chakula na mifumo ya afya, pamoja na kijamii, ikiwamo ya kijinsia na athari hizo kwa kiasi kikubwa zimesababisha mafuriko, ukame, kuenea kwa mimea vamizi, kuongezeka kwa usawa wa bahari na maporomoko ya ardhi ni miongoni mwa matokeo yanayoonekana zaidi ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa bahati mbaya na kusababisha athari kwa makundi ya wanawake, vijana na watoto.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk. Ashati Kijaji, alisema mabadiliko ya hali ya hewa huleta hatari zinazojidhihirisha kupitia hali mbaya ya hewa, kupanda kwa joto, mvua zisizotabirika, dhoruba za kitropiki na mafuriko ambayo yameathiri uchumi na ikolojia wa jamii.

Alisema changamoto hizo husababisha hasara na uharibifu wa miundombinu muhimu, kutoka barabara na madaraja, huduma, njia za umeme kutishia huduma muhimu zinazotegemea maisha na kusababisha uhaba wa maji na upungufu chakula.

Aidha, dhoruba za kitropiki kama vile hidaya, tayari zimeharibu miundombinu ya makazi na usambazaji wa umeme, haswa katika Wilaya za Kilosa na Mvomero huko Morogoro na Zanzibar, kuna ulazima wa uhitaji wa dharura wa kuchukua hatua kabambe ya hali ya hewa ikiwamo kujenga uwezo wa kustahimili mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema miongoni mwa mambo mengi ni mishtuko ya mambo ya ndani na nje yanayohusu mabadiliko ya hali ya hewa katika kukabiliana na hali ya ustahimilivu.