Wanaohisi wanyonge kijamii rahisi kujitoa uhai-Dk.Masao

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:03 PM Sep 11 2024
Bingwa Mshauri Mwandamizi wa Magonjwa ya Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Frank Masao
Picha: Christina Mwakangale
Bingwa Mshauri Mwandamizi wa Magonjwa ya Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Frank Masao

WATU wenye wasiwasi, wanaojitenga, waraibu wa vilevi na wanaojihisi wanyonge katika jamii kama vile wakimbizi ni miongoni mwa wanaotajwa kuwa hatarini katika kutoa uhai.

Bingwa Mshauri Mwandamizi wa Magonjwa ya Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Frank Masao, aliyasema hayo Septemba 10, mwaka huu, ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Uzuiaji Kujiua Duniani. 

Alisema makundi matatu kwenye jamii ikiwamo wanaojihisi unyonge, waliofanyiwa ukatili na vijana katika umri wa miaka 15 hadi 29, wamo hatarini kuingia katika hatari hiyo.

“Mara nyingi maneno yakawa mchakato wa mtu kutaka kujitoa uhai, atatamka maneno hayo kwa utani au masihara. Kujitenga, kutawanya mali zake bila sababu za msingi na kubadili tabia zake ni dalili,” alisema Dk. Masao.

Alisema kwamba watu wa aina hiyo na wenye dalili hizo wanaweza kupatiwa ushauri, kuwatibu kiakili kutokana na madhila wanayopitia na changamoto mbalimbali maishani.

“Changamoto za watu hawa mara nyingi zinaendana na tatizo la akili. Wanaohitaji usaidizi wa kisaikolojia na kuiepusha jamii kwenye matukio hayo,” alieleza Dk. Masao.

Alitoa wito kwa jamii kutokaa na sumu za aina tofauti kama vile za wadudu na kwamba dawa za mazao na binadamu zihifadhiwe mahala ambako hapafikiwi haraka, ili inapotokea mmoja wa wanafamilia akitaka kutenda tukio hilo isiwe rahisi.