WANAFUNZI 12 wa Shule ya Sekondari Ipandikilo iliyoko Kata ya Ngoma ‘B’ wilayani Sengerema mkoani Mwanza wanadaiwa kuchapwa viboko 75 kwa kila mmoja.
Hali hiyo imewasababishia kupata majeraha na kulazimika kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Ngoma ‘B’.
Wanafunzi hao wanadaiwa kuchapwa viboko hivyo baada ya kukutwa na makosa ya kinidhamu ikiwemo kujihusisha na mapenzi shuleni kinyume na sheria za shule.
Mkuu wa shule hiyo, John Paulo akielezea tukio hilo juzi alisema wanafunzi hao waliadhibiwa na baadhi ya walimu shuleni hapo na yeye alikuta tayari wameumizwa sehemu mbalimbali za miili.
Alisema alilazimika kuwapeleka katika kituo cha afya ili wakapate matibabu na vipimo wakisaidiana na Mtendaji wa Kata.
Ofisa Mtendaji Kata wa Ngoma ‘B’, Emili John alithibitisha kupokea taarifa za malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao.
Alisema baada ya kupokea malalamiko hayo alimuuliza Mkuu wa Shule ambaye alimweleza kuwa ilikuwa sehemu ya adhabu ya utovu wa nidhamu na tayari walimu wamechukuliwa hatua ikiwemo kukanywa juu ya kutolewa kwa adhabu za namna hiyo.
Akithibitisha kuwapokea wanafunzi hao, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ngoma ‘B’, Abutwale Bukwaje alisema wanafunzi waliopokelewa kituoni hapo ni 12 ambao walibainika kuwa na michubuko katika sehemu mbalimbali za miili yao.
Diwani wa Kata hiyo, Donald Masinde alisema kitendo hicho hakiwezi kuvumiliwa na kukitaja kama sehemu ya ukatili na unyanyasaji kwa wanafunzi, huku akiahidi kuhakikisha wote waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilayani Sengerema, Jackson Mazinzi alilaani kitendo cha wanafunzi kuadhibiwa kikatili na walimu hao na kuwataka kuzingatia sheria za utoaji adhabu shuleni.
Hivyo, alimwagiza Mkuu wa Shule hiyo kuwaeleza walimu wake namna sahihi ya kutoa adhabu kwa wanafunzi na siyo kuwachapa viboko visivyo na idadi na kusema suala hilo kuwa kinyume maadili ya ualimu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED