TRA, BASATA kubaini wasanii walipaji, wasiolipa kodi

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 11:02 AM Dec 25 2024
Katibu Mtendaji BASATA, Dk. Kedmon Mapana (kushoto), akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuphu Mwenda.
Picha: Pilly Kigome
Katibu Mtendaji BASATA, Dk. Kedmon Mapana (kushoto), akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuphu Mwenda.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), wameingia makubaliano ya kubadilishana taarifa na kusomana katika mifumo ya kudhibiti mapato yatokanayo na wasanii, ikiwamo kubaini wasanii wanaolipa na wasiolipa kodi nchini.

Kamishna wa TRA, Yusuphu Mwenda alisema hayo mbele ya vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam kuwa makubaliano hayo yatawezesha kusomana mifumo, kati ya TRA na BASATA katika ukuzaji na kuendeleza sekta ya sanaa nchini.

Alisema hiyo ni katika utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kutaka taasisi za umma, makampuni kusomana kwa taarifa.

Alisema mifumo hiyo itaweza kubaini na kutambua ni wasanii gani na wangapi wamesajili na TRA na kujua ambao hawajasajiliwa, ili waweze kuwasaidia kutambulika kuwasajili na kupata TIN namba kwa gharama kidogo.

Alifafanua msaniii atakayekuwa na mapato ya chini ya Sh. 170,000 serikali imemsamehe, atakayekuwa na mapato yatakayozidi hapo atachangia kiasi kidogo.

TRA, BASATA kubaini wasanii walipaji, wasiolipa kodi
Alisema msanii atakayeanzisha kampuni yake akiwa na mapato chini ya Sh. milioni nne kwa mwezi, atasamehewa kulipa kodi lakini akiwa na mapato kwa mwaka kuanzia Sh. milioni saba, atachangia laki moja kwa mwezi na yule atakayekuwa na mapato ya Sh. milioni saba hadi Sh. milioni 11 atalipa kwa mwezi Sh. 250,000.

Pia akiwa na mapato kuanzia Sh. milioni 11 hadi 100 kwa mwezi, atachangia asilimia 3.5 ya kile anachoingiza.

Katibu Mtendaji BASATA, Dk. Kedmon Mapana alisema mifumo itaeta mapinduzi na mabadiliko makubwa katika sekta ya sanaa, kwa wasanii wote wakiwamo waimbaji, wachoraji, MC, wachongaji na wengine wote wanaoingia kwenye kundi hilo.

Alisema watakwenda kuipa serikali mwamko ya kuisaidia sekta hii kwa kuwa wasanii wanalipa kodi, ikiwamo mifumo itaenda kusaidia wasaniii na wadau wa sanaa kufanya shughuli zao bila bugudha.