MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema sababu ya kuongezeka kwa joto katika baadhi ya maeneo nchini ni kutokana na kusogea kwa jua la utosi na upungufu wa mvua katika maeneo yanayopata misimu miwili kwa mwaka.
Mikoa hiyo inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Zanzibar, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Geita, Kagera, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na TMA, jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine.
"Kwa kawaidi vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kileleni mwishoni mwa Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kasakazini (tropiki ya kansa)," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ilisema katika kipindi cha Februari, mwaka huu, hali ya ongezeko la joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini. Hadi kufikia Februari 11, mwaka huu, kituo cha hali ya hewa cha Mlingano (Tanga) kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 36°C ikiwa ongezeko la nyuzi joto 2.1°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa Februari.
Pia kituo cha hali ya hewa kilichoko katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kiliripoti kiwango cha juu cha nyuzi joto 35.0°C Februari 10 , 2025 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 2.2°C.
Kituo cha Kibaha siku hiyo kiliripoti nyuzi joto 35.8 °C ikiwa ongezeko la nyuzi joto 3.0°C huku kituo cha Kilimanjaro kikiripoti nyuzi joto 34.3°C Februari 9 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 0.6°C.
Kutokana na ongezeko la joto, wataalamu wa afya wameshauri wananchi wa maeneo tajwa kunywa maji na vimiminika vingine kama sharubati kwa wingi.
Dk. Milagilo Malombe kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) - Mloganzila, alisema kipindi hiki cha joto watu hupoteza maji mengi, hivyo ni vizuri kuweka utaratibu wa kunywa maji kwa wingi.
Pia ameshauri watu kuvaa nguo nyepesi zisizochochea hali ya joto kali.
"Lakini pia kipindi hiki magonjwa ya ngozi huibuka kwa wingi, wadudu kama fangasi wanaibuka sana nashauri watu kudumisha usafi kwa kuoga mara kwa mara na kujikausha maji. Hii itasaidia kuepuka magonjwa ya ngozi," alisema Dk Milagilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED