Serikali yaweka ngumu uraia pacha

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:57 AM Apr 19 2024
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashari, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.
PICHA: MAKTABA
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashari, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.

SERIKALI imesema bado haiko tayari kuwa na utaratibu wa kutoa uraia pacha badala yake iko katika hatua za mwisho kukamilisha utoaji wa hadhi maalum kwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania, ili kuwezesha kuchangia maendeleo ya taifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashari, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, amesema hayo jijini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafaniko ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano.

“Mchakato huo unatarajiwa kukamilika baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kukamilisha kufanya marekebisho ya Sheria za Ardhi na Uhamiaji ndipo hadhi maalum itaanza kutumika rasmi,” amesema Balozi Mbarouk.

Aidha, amesema wizara imekamilisha mfumo wa kidijitali wa kukusanya na kutunza taarifa za diaspora unaofahamika ‘Diaspora Digital Hub’.

“Mpaka sasa diaspora wa Tanzania wapatao 1,403 wamejiandikisha katika mfumo huo na hivyo kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi za idadi, mahali walipo, ujuzi na uzoefu walionao.

“Mfumo pia utawezesha diaspora kupata taarifa kuhusu fursa na huduma mbalimbali zinazotolewa na serikali na sekta binafsi nchini, lakini pia mfumo huu unawasaidia kuwapunguzia usumbufu wa kwenda kwenye balozi au kutuma barua kwa ajili ya kujiandikisha,” amesema.

Kadhalika, amesema katika kipindi hiki cha miaka 60 ya Muungano serikali imefanikiwa kuimarisha ushiriki wa Watanzania waishio nje ya nchi raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania katika maendeleo ya taifa.

Amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni serikali kuchukua hatua za kisera kwa kujumuisha masuala ya diaspora katika mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001.

“Katika kipindi hiki, Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kulinda amani duniani kama hatua ya utekelezaji wa malengo ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje na mojawapo ya malengo mahsusi ya Umoja wa Mataifa (UN),” amesema.

Amesema Tanzania imekuwa ikishiriki katika kulinda amani kupitia Misheni za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Amesema baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imechangia walinda amani ni pamoja na Lebanon, Darfur, Abyei, Liberia, Sudan Kusini, Sudan, DRC, Msumbiji na Afrika ya Kati.

“Kwa upande mwingine, Tanzania imeshiriki kikamilifu utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo na diplomasia kwenye nchi na maeneo mbalimbali ikiwamo, Darfur, Cambodia, Sudan Kusini, Burundi na Kenya,” amesema.