Sakata wodi lazua kizaazaa bungeni

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:40 AM Aug 28 2024
MBUNGE wa Ilemela (CCM), Dk. Angelina Mabula.
Picha:Mtandao
MBUNGE wa Ilemela (CCM), Dk. Angelina Mabula.

MBUNGE wa Ilemela (CCM), Dk. Angelina Mabula, ameibua sakata jipya bungeni:

Katika siku ya kwanza ya mkutano wa Bunge jana, alisema Kituo cha Afya Sangabuye, Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza kina wodi moja inayotumiwa na wanaume, wanawake na watoto. 

Kutokana na hoja hiyo ya mbunge, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameelekeza Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itafute taarifa kwa kina kuhusu suala hilo na kutolea ufafanuzi bungeni - watu hao wanalalaje katika wodi moja ili jambo hilo likae vizuri katika taarifa za Bunge. 

Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, mbunge huyo alisema kituo hicho kimetokana na kupandishwa hadhi kutoka zahanati na kuwa kituo cha afya mwaka 1999, lakini hadi sasa kina wodi moja inayotumiwa na wanawake, wanaume na watoto na kuhoji ni lini serikali itakamilisha majengo ya kituo hicho pamoja na kujenga uzio. 

"Katika kituo hicho, kitanda kimoja unakuta amelazwa mwanamke na kinachofuata, mwanamume na kingine mwanamke ana mtoto, na ni kutoka mwaka 1999 miundombinu haijakamilika," alisema. 

Kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Dk. Festo Dugange, Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson alionesha kushtushwa na jambo hilo na kumhoji mbunge Mabula: 

"Mheshimiwa Angelina Mabula; watoto, wanawake na wanaume wanalazwa katika wodi moja?" 

Mbunge huyo akajibu, "Kweli Mweshimiwa Spika". Spika Tulia akauliza tena, "Wanawezaje kwa wodi moja, ninapata shaka, yaani wameweka mapazia au nini?" 

Akitoa ufafanuzi kuhusu hilo, Mbunge Mabula alisema, "Katika kituo hicho cha afya unaweza ukakuta kitanda kimoja amelazwa mwanamke, kitanda kinachofuata kuna mwanamume na kingine kuna mwanamke mwenye mtoto, ndani ya wodi moja na ni tangu 1999 miundombinu hiyo haijakamilika." 

Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Dk. Dugange, alisema kuwa kwa mujibu wa utaratibu na Sera ya Afya, hairuhusiwi kulaza wagonjwa wa jinsia tofauti katika wodi moja. 

"Kwa taarifa hii, TAMISEMI tunaipokea kwamba kuna tatizo katika uongozi wa hospitali hiyo na manispaa yenyewe. 

"Ninaomba Mheshimiwa Spika nichukue hoja hii nimwelekeze Mkurugenzi wa Manispaa leo (jana) hii afike pale mara moja na atupe taarifa rasmi TAMISEMI, ili kuona namna nzuri ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaolazwa kwa kuwa haikubaliki kulaza wanawake na wanaume wodi moja," alisema. 

Dk. Dugange pia alimwagiza Mkurugenzi wa manispaa hiyo kupitia mapato ya ndani kuanza ujenzi wakati TAMISEMI ikitafuta fedha kwa ajili ya kuwaunga mkono. 

Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Dk. Alfred Kimea, alihoji lini Kituo cha Afya Mgombezi kitapatiwa fedha iliyobaki Sh. milioni 250 ili kumalizia ujenzi wake. 

Akijibu swali hilo, Dk. Dugange alisema katika mwaka wa fedha 2021/22, serikali iliipatia Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Sh. milioni 250 kwa ajili ya kuipandisha hadhi Zahanati ya Mgombezi kuwa kituo cha afya. 

 "Fedha hizo zimejenga wodi ya wazazi na jengo la upasuaji ambapo, jengo la wazazi tayari limekamilika na linatumika. Jengo la upasuaji lipo katika hatua ya umaliziaji ambapo zinahitajika Sh. milioni 36 kulikamilisha," alisema. 

Naibu Waziri huyo alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe itakitengea Sh. milioni 36 kwa ajili ya

ukamilishaji jengo la upasuaji na serikali itatenga Sh. milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu iliyosalia.