Polisi yapiga marufuku maandamano CHADEMA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:42 AM Sep 14 2024
Msemaji wake, Naibu Kamishna (DCP) David Misime
Picha:Mtandao
Msemaji wake, Naibu Kamishna (DCP) David Misime

WAKATI Jeshi la Polisi likionya maandamano yaliyopangwa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa atakayeshiriki atakabiliwa vilivyo, wenyewe wamelitunishia ‘misuli’ jeshi hilo kwa kueleza kuwa ratiba iko pale pale.

Jana, Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, Naibu Kamishna (DCP) David Misime, lilionya yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo.

Kauli hiyo imetolewa baada ya chama hicho siku mbili zilizopita kuwaita makada wake kutoka mikoa mbalimbali kwenda Dar es Salaam kushiriki maandamano.

CHADEMA imetangaza kuanzia Septemba 23, mwaka huu, wataanza kuingia barabarani kushinikiza viongozi kadhaa kujiuzulu kutokana na mauaji ya Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho, Ally Kibao.

 Akizungumza jana na waandishi wa habari katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi, mkoani Kilimanjaro, DCP Misime alionya chama hicho kuacha kuendelea kuhamasisha wananchi kujihusisha katika uhalifu huo na atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Hatua hiyo waliyofikia (CHADEMA) tunajiuliza na tunaendelea kufuatilia na uchunguzi kwa nini wanataka kututoa kwenye reli ya hatua za kiupelelezi zinazoendelea, baada ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan, kuelekeza au kuagiza vyombo vifanye uchunguzi kisha kuwasilisha taarifa kwake,” alisema DCP Misime.

Alisema mara kadhaa viongozi na wafuasi wa chama hicho wamekuwa wakipanga, kuratibu mikakati mbalimbali na kutoa matamshi yenye lengo la kutaka au la kuleta vurugu nchini, ili kuharibu amani ya nchi kwa sababu wanazozijua wao wenyewe.

DCP Misime alisema Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa viongozi wa chama hicho, kuacha kuendelea kuhamasisha wananchi kujihusisha katika uhalifu huo, na yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Kwa maana hiyo, maandamano hayo yamepigwa marufuku. Jeshi la Polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo asithubutu kufanya hivyo, kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika.

“Hivyo asipoteze muda na gharama yake. Jeshi la Polisi Nchini, linaendelea kutoa rai kwa wananchi wapenda amani kutokubali kurubuniwa, kudanganywa au kushawishiwa kwa namna yeyote ile kushiriki katika maandamano hayo na badala yake waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani,” alisema.

CHADEMA YAJIBU 

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alipoulizwa na Nipashe kuhusu onyo hilo, alisema msimamo wao ni kwamba,maandamano yaliyopangwa yako palepale.

“Tutatoa ratiba wapi yanaanzia na kuishia. Msemaji wa Polisi si mamlaka halali ya kuzuia maandamano yetu. Sheria inamtambua Mkuu wa Polisi Wilaya husika na sisi tutafuata sheria kuliarifu Jeshi la Polisi kwa sababu mpaka sasa hatujaliarifu maandaamano yetu yataanzia wapi na kwenda wapi,” alisema.

Mrema alisema mpaka Septemba 21, mwaka huu, endapo watakuwa hawajawaachia watataarifu rasmi maandamano hayo.

“Kauli ya msemaji wa Jeshi la Polisi tunaichukulia kama kauli nyingine lakini kwa mujibu wa sheria hana mamlaka ambayo amejipa kwa mujibu wa sheria yenyewe ya Jeshi la Polisi lenyewe,” alidai.

Septemba 11, mwaka huu, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, akiwa Mikocheni mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache baada ya maziko ya Kibao alinukuliwa akisema:

“Nimetangaza hadi kufikia Septemba 21, mwaka huu, tunategemea tuone hatua za watu kuwajibika kuwarejesha waliotekwa na viongozi kadhaa kujiuzulu.

“Kama hawatochukuliana hatua wenyewe kwa wenyewe sisi kuanzia Septemba 23, 2024 jiji lote la Dar es Salaam kila kata kila mtaa, wawe tayari.

“Ndugu zangu tumekuwa tunafanya utani mara nyingi ‘this time around’ hatuna utani, kuanzia Jumatatu Septemba 23, mwaka huu, sisi tutaingia barabarani kudai uhai wa watu wetu waliopotezwa ‘unless’ serikali ichukue hatua za haraka na za makusudi kuwarejesha watu, kujiuzulu na watu wote kuwajibika,” alisema.

Aidha, Mbowe alisema kabla ya maandamano hayo Kamati Kuu ya CHADEMA itakutana Septemba 16 na 17, kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwamo utekaji, mauaji na kupotea kwa viongozi wao.

·         Imeandikwa na Godfrey Mushi (MOSHI) na Romana Mallya (DAR)