Manung’uniko ya malipo, lawama ubomoaji nyumba Bonde Msimbazi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:34 AM Apr 17 2024
Mkazi wa eneo la Jangwani, Kata ya Mchikichini, Zahor Mohamed (mwenye kanzu nyeusi), akisimamia ubomoaji wa nyumba yake, ili kupisha Mradi wa Bonde la Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
PICHA: ROMANA MALLYA
Mkazi wa eneo la Jangwani, Kata ya Mchikichini, Zahor Mohamed (mwenye kanzu nyeusi), akisimamia ubomoaji wa nyumba yake, ili kupisha Mradi wa Bonde la Msimbazi, jijini Dar es Salaam.

BOMOA bomoa nyumba kupisha Mradi wa Bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam inaendelea, huku baadhi ya wakazi wakilalamikia fidia ndogo na wapangaji wakirusha lawama kwa wenye nyumba kuchukua fedha za pango, huku wakiwa wameshachukua malipo ya kuondoka.

Wapangaji wamelalamikia wenye nyumba kuchukua kodi za nyumba wakati wakiwa wametia saini serikalini malipo ya kuondoka maeneo hayo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wakati wananchi wakiendelea na ubomoaji wa nyumba zao baada ya fidia, walisema malipo yalivyofanyika yamekuwa na sintofahamu kwao.

“Binafsi sijakataa kuondoka. Nimesaini fedha, lakini kiuhalisia fedha niliyosaini haina thamani ya ardhi yangu na nyumba yangu ninayovunja yenye vyumba vitano,” amesema Thobias Hiporiti, mkazi wa Kata ya Mzimuni, Mtaa wa Mwinyimkuu, Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.

Hiporiti amedai awali wakati wanaelezwa kuhusu kuwapo kwa mradi huo, waliambiwa watakaopisha watapewa fedha si chini ya Sh. milioni 70, lakini ameshangaa wakati akitia saini fidia yake ameambulia Sh. milioni 34 wakati ana hati ya eneo hilo.

“Mimi nipo tofauti na wenzangu. Nina hati ya ardhi na nimekuwa nikiilipia kila mwaka. Machi 14, 2023, nilipata fidia ya awamu ya kwanza Sh. milioni 26.5.

“Novemba 2, 2023, nikapata nyongeza ya zaidi ya Sh. 800,000 na hii ni baada ya baadhi ya wananchi kugomea malipo yao kuwa ni madogo. Baadaye tena nikapewa Sh. milioni nne ambazo niliambiwa Rais ameongeza fedha hii.

“Kwa ujumla tunaondoka hapa kinyonge. Baada ya kusaini malipo nilipewa muda wa kuondoka hapa hadi Aprili 12, 2024, muda umeisha ndiyo naendelea kubomoa nyumba yangu kidogo kidogo angalau niondoke na baadhi ya vitu ambavyo vitanisaidia huko mbele badala ya kusubiri kubomolewa,” amesema.

Kibagu Juma, mkazi wa eneo hilo, amesema nyumba yao ina vyumba vitano, licha ya kupewa malipo bado hajaanza kubomoa.

“Nilishasaini fidia tangu Aprili 8, mwaka huu, ninasubiri iingie katika akaunti yangu ndipo nianze kubomoa kidogo kidogo nyumba.

“Kwa ujumla fedha niliyopewa ni kidogo nimefidiwa Sh. milioni 20, nyumba hii ilikuwa ya wazazi wetu ambao walishafariki dunia, watoto tumebaki wawili.

“Hapa kuna kugawana tena Sh. milioni 10 kila mmoja. Sasa Sh. milioni 10 unaifanyia nini kwa maisha ya sasa. Kwanza maeneo tu ya hapa tangu mchakato huu utangazwe vyumba vimepanda bei, na bei ya viwanja huko mnaijua,” amesema.

Imani Mwangunga, mkazi wa Kata ya Mchikichini, amesema nyumba yake ambayo alianza juzi kuibomoa ina vyumba vinane na vyoo viwili vya ndani na ipo ndani ya uzio.

“Nimefidiwa Sh. milioni 51 ambapo Sh. milioni 47 ni fidia ya nyumba na Sh. milioni nne fidia ya ardhi. Nikiitazama nyumba hii na nilichofidiwa nikiangalia na gharama za maisha kwa sasa vitu vimepanda bei, ninaona bado sikustahili fedha ilipaswa iwe zaidi,” amesema.

Mwangunga amesema katika malipo hayo pia, amefidiwa migomba iliyoko katika ua wake Sh. 175,000, lakini choo cha nje pamoja na uzio hajafidiwa chochote.

Amesema ameanza kubomoa nyumba hiyo kwa kuwa amepewa wiki sita za kuondoka hapo tangu asaini fidia hiyo.

Zahor Mohamed, mkazi wa Kata ya Mchikichini, Jangwani jijini Dar es Salaam ameonesha kuridhishwa na fidia hiyo ingawa kutokana na gharama za vifaa vya ujenzi sokoni hivi sasa, lakini amesemaserikali ilipaswa kuiangalia ili kuondoa manung’uniko.

Amesema nyumba anayobomoa bila kutaja fidia yake, ni yenye vyumba tisa.

Mpangaji Veronica Mdugala, anayeishi eneo la Madaba, Kata ya Mzimuni, amesema alipanga vyumba viwili na amekaa kwa miaka mitano.

“Mwenye nyumba hajatuambia kama ameshalipwa fidia, Nimelipa kodi Aprili 2, mwaka huu, kwa ajili ya mwezi Machi na Aprili, sasa ametupa siku mbili tundoke. Hapa tupo wapangaji wanne yeye hakai hapa,” amesema.

Mpangaji huyo alidai kuwa tangu mchakato huo uanze, vyumba katika maeneo yanayozunguka bonde hilo vimepanda bei kutoka Sh. 50,000 kwa chumba hadi Sh. 80,000.

Serikali ilitangaza kuanza rasmi kwa mradi huo Jumatatu wiki hii, ukisimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini Tanzania (TARURA).