Mwenge kugusa miradi ya trilioni nane Pwani

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:29 PM Apr 30 2024
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru tayari kuukimbiza mkoani kwake.
Picha: Julieth Mkireri
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru tayari kuukimbiza mkoani kwake.

MWENGE wa Uhuru 2024 umepokelewa katika Mkoa wa Pwani ukitokea mkoani Morogoro na unatarajia kukimbizwa Km 1,225.3 ambapo utakagua, utazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 126 yenyewe thamani ya zaidi ya sh trilioni nane.

Mwenge huo umepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, katika eneo la Bwawani kata ya Ubena Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo.

Aidha, makabidhiano hayo pia yameshuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Pwani akiwemo mke wa Rais Mstaafu awamu ya nne Mama Salma Kikwete pamoja na Mbunge wa Chalinze Ridiwani Kikwete.

Akizungumza katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, Kunenge amesema thamani ya miradi ya mwaka huu ni zaidi ya miradi ya mwaka 2023 ambayo ilikuwa na thamani ya Sh. Trillioni 4.4.

Amesema miradi 18 itawekwa mawe ya msingi, 22 itakaguliwa na 16 itazinduliwa na kwamba mafanikio ya uwepo wa miradi hiyo yametokana na uwekezaji na fedha zilizotolewa na Serikali.

Kunenge amesema adhma ya  Mkoa huo ya kutunza mazingira umelenga kupanda miti milioni 13.5 hadi kufikia mwezi June 2024 katika kipindi cha mwaka 2013/2024 na hadi sasa miti milioni 8,884,935 imepandwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, amesema utakimbizwa katika Halmashauri mbili Chalinze na Bagamoyo na miradi 29 yenyewe thamani ya sh. bilioni 15.2 itapitiwa.

Katika Halmashauri ya Chalinze kati ya miradi iliyopitiwa na Mwenge ni pamoja na daraja Kijiji Cha Visakazi kata ya Ubena namna ulivyoakiso matumizi sahihi ya rasilinali fedha za umma na Wahisani.