DC Mhita apiga marufuku vifungashio visivyo rasmi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:03 PM Apr 30 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akiwa ameshika vifungashio vilivyopigwa marufuku katika soko Kuu la Namanga.
Picha: Shabam Njia
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akiwa ameshika vifungashio vilivyopigwa marufuku katika soko Kuu la Namanga.

MKUU wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kufanya msako na kuwakamata wafanyabiashara wanaoingiza vifungashio vya mifuko vilivyopigwa marufuku na serikali na kuviuza kinyemela kwa wajasiriamali wadogo.

Mhita ametoa agizo hilo wakati akiongoza wakazi wa wilaya ya kahama kufanya usafi wa Mazingira katika soko kuu la manispaa ya Kahama maarufu kama Namanga, huku akiwasisitiza suala la usafi kufanyika kila siku ili kulinda afya ya watumiaji wa bidhaa wanazouza.

Amesema, hakuna viwanda vya ndani vinavyozalisha vifungashio vilivyopigwa mafurufu na serikali na vingi vinavyoingia vinazalishwa nchi za jirani na kuingizwa kinyemela na wafanyabiashara wetu ambao wanawauzia wajasiriamali wadogo na kufungia bidhaa zao hivyo wanatakiwa kuachama mara moja kabla ya kuanza kuwajibishwa.

Naye Ofisa Afya na Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Johannes Mwebesa amesema, kwa mfanyabishara atakayekamatwa anafunga bidhaa zake kwa vifungashio vilivyopigwa marufuku atatozwa faini ya Sh.30,000 fedha ambayo ni kubwa na itashusha mtaji wake.

Amesema, na wengi wao wanavitumia kufunga bidhaa ya karanga zilizosangwa, mbaazi, karanga ambazo hazijasagwa na mambo mengine na kuwataka kutoa taarifa wanapotoa vifungashio hivyo kabla ya kuanza msako na kuwabaini kwani hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaobainika.

Hoja hiyo iliibuliwa na mmoja wa wafanyabishara wa soko hiloElizabeth Silvester aliyelalamika kuwepo kwa vifungashio vilivyopigwa marufuku na vimekuwa vikisambaa ovyo sokoni na kuchafua mazingira hali iliyowaibua viongozi wa serikali kupita marufu na kuagiza kuanza kwa msako wake chini ya kamati ya ulizi na usalama.