Diwani awaonya wananchi kuhusu madalali wa kisiasa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 03:06 PM Apr 30 2024
Diwani wa Kata ya Kindai, Manispaa ya Singida, Omary Kinyeto.
PICHA: MAKTABA
Diwani wa Kata ya Kindai, Manispaa ya Singida, Omary Kinyeto.

DIWANI wa Kata ya Kindai, Manispaa ya Singida, Omary Kinyeto, amewataka wananchi wa kata hiyo kujiepusha na madalali wa kisiasa wanaowarubuni kwa kuwachafua viongozi waliopo madarakani ili wasiwachague katika chaguzi zijazo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara ambao aliutumia kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kinyeto amesema endapo wakirubuniwa na madalali hao itasababisha kuchagua viongozi ambao hawawezi kutatua changamoto zao kwa kipindi cha miaka mitano.

Amesema ni muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi ambao watasaidia kuleta maendeleo katika kata yao na siyo kuchangua viongozi ambao wanajali maslahi yao binafsi na familia zao.

Aidha, Kinyeto ameishukuru serikali kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inasaidia wananchi kupata huduma za kijamii katika maeneo yao.

Kuhusu suala la barabara, amesema serikali inaendelea kutenga fedha za kujenga na kukarabati barabara za kata hiyo, ili ziweze kupitika muda wote.

Kinyeto  amesema endapo barabara zitapitika muda wote itarahisisha usafirishaji wa bidhaa na wananchi kuweza kufuata huduma za kijamii kwa urahisi.

Diwani huyo ameongeza kuwa katika kata hiyo serikali inatarajia kujenga barabara kwa kiwango cha lami na hivyo wananchi waendelee kutoa ushirikiano pale wanapohitajika.

Kuhusu elimu, Kinyeto  amesema serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga madarasa katika shule ambazo zilikuwa na upungufu wa madarasa katika Kata ya Kindai.

Hivyo, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata elimu, akisema ni haki yao ya msingi.

Aidha ametoa msaada wa viti 207 na sahani 660 kwa Kata ya Kindai kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii pale zinapojitokeza ili wananchi kuepuka gharama za kukodi vifaa hivyo.