Mabadiliko Sheria ya TAKUKURU, faini makosa rushwa ya ngono kuongezwa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:57 AM Sep 03 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

MUSWADA wa marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2024, umependekeza kuongeza kosa na adhabu ya rushwa katika uchaguzi, michezo, michezo ya kubahatisha na burudani.

Lengo la marekebisho hayo ni kuiwezesha Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia rushwa katika uchaguzi, michezo, michezo ya kubahatisha na burudani.

Hayo yalisemwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, wakati akiwasilisha maelezo ya muswada huo.

“Lengo la marekebisho haya ni kuiwezesha taasisi kupambana na rushwa kufanyakazi kwa ufanisi katika nyanja hizi na hivyo kuhakikisha uadilifu na haki vinadumishwa katika michakato ya uchaguzi, matukio ya michezo, shughuli za michezo ya kubahatisha na tasnia ya burudani,” alisema.

Aidha, alisema adhabu ya faini isiyopungua Shilingi milioni mbili na isiyozidi Sh. milioni 10 au kifungo kisichopungua miaka mitano imewekwa kwenye makosa ya rushwa ya ngono katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2024.

Alisema kifungu cha 25 kinaweka masharti kuwa ni kosa kwa mtu mwenye mamlaka kuomba rushwa ya ngono au kuomba upendeleo wa aina nyingine kama sharti la kutoa au kupata ajira, cheo, haki au upendeleo mwingine wowote.

Pia alisema kinaeleza kuwa ni kosa kwa mtu anayeahidi au kutoa rushwa ya ngono au upendeleo mwingine kwa mtu mwenye mamlaka au aliye katika nafasi ya mamlaka ili kumshawishi mtu huyo kutoa upendeleo wa ajira, cheo, haki au upendeleo mwingine wowote. 

USHAURI WA KAMATI

Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mjumbe wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki, alisema mapendekezo ya mabadiliko ya sheria katika kifungu cha 25 hasa ongezeko la kifungu kipya cha 25(1) (b) kimeleta hisia hasi kwa wadau waliofika mbele ya kamati, asasi za kiraia na wanaharakati mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Wadau wengi wamelalamikia kifungu hicho kwa mtazamo kuwa kinawanyima waathirika wa rushwa ya ngono haki zao stahiki na kinawapa kinga wahusika wa vitendo hivyo,” alisema.

Alisema kuwa kamati ilibaini kuwa chimbuko la mapendekezo hayo ni pamoja na mikataba ya Kimataifa na Kikanda, Ibara ya 15(a) ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa inaelekeza nchi wanachama kutunga Sheria yenye kosa la kushawishi kutoa rushwa ya ngono, Ibara ya 4 (1) (b) ya Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa inaelekeza nchi wanachama kutunga sheria yenye kosa la kushawishi kutoa rushwa ya ngono.

Pia, alisema Ibara ya 3 (b) ya Mkataba wa SADC dhidi ya rushwa inaelekeza nchi wanachama kutunga sheria yenye kosa la kushawishi kutoa rushwa ya ngono.

“Hapa nchini, Tanzania Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi kwenye Sheria ya 14 Kupambana na Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi ya Mwaka 2023 kifungu cha 52 kimeainisha kuwa ni kosa kushawishi kutoa rushwa ya ngono.”

“Kamati ilijiridhisha kuwa kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, sura ya 329 imeainisha kuwa ni kosa kwa mtu yeyote ambaye atatoa au ataahidi kutoa rushwa kwa namna yoyote ile ili kupata upendeleo wowote mtu huyo atakuwa ametenda kosa la rushwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema ili kuweka mkazo kwa mtu mwenye mamlaka kutoshawishika kutoa upendeleo wa aina yoyote kwa ahadi ama kupewa rushwa ya ngono. Kamati inapendekeza kuongeza adhabu kwenye kifungu cha 25 cha sheria hiyo, kwa adhabu ya faini ukomo wa juu kutoka kuwa Shilingi milioni tano na kuwa Sh. milioni 10, na kwa adhabu ya kifungu ukomo wa juu kutoka kuwa miaka mitatu na kuwa miaka 10.