Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana, amesema Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela ni mmoja wa viongozi waliopata mafanikio makubwa katika uongozi nchini, Afrika Mashiriki na duniani kwa ujumla.
Kinana ameyasema hayo jijini Dodoma katika hafla ya kumbukizi ya kuzaliwa Mzee Malecela iliyofanyika nyumbani kwake Mtaa wa kilimani. Mzee Malecela amesherehekea kutimiza umri wa miaka 90.
"Watu waliopata bahati ya kulelewa na mzee Malecela katika uongozi ni pamoja na mimi. Mzee Malecela ana uzalendo mkubwa na serikali hii.
"Ni mzee mwenye busara, kwa kauli ya haraka ukimuacha Baba wa Taifa (Hayati Mwalimu Julius Nyerere), Ali Hassan Mwinyi (Hayati Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili), kiongozi pekee aliyepata nafasi ya kuhudumia Afrika Mashariki, Afrika na duniani Hadi kuwa mtu mashuhuri duniani ni Mzee Malecela," amesema Kinana.
Kinana amesema moja ya sifa ya Malecela anajua kupima ni wakati gani wa kuchukua hatua gani, na wakati gani wa kufanya maamuzi, ndio maana ameendelea kuheshimika.
"Mzee Malecela Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatambua mchango wako katika kukijenga Chama hiki. Nakupongeza kwa kutimiza miaka 90, Mwenyezi Mungu tunamuomba akupe umri wa ziada," amesema Kinana
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED