Jaji: Daktari huyu afunguliwe kesi ya jinai

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:49 AM Jun 27 2024
Daktari.
Picha: Maktaba
Daktari.

JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Hamidu Mwanga, ameshauri Dk. Martha Tsere, ambaye anadaiwa kughushi fomu ya bima ya maisha ya rafiki yake wa karibu, afunguliwe kesi ya jinai.

Dk. Matha anadaiwa kughushi fomu ya bima ya maisha ya rafiki yake, marehemu Tarsila Oisso, akidai kuwa anatakiwa apewe asilimia 40 ya bima hiyo.

Katika shauri hilo la madai namba 11290 la mwaka 2024, mlalamikaji ni Shirika la Usimamizi wa Maendeleo kwa Afya (MDH) na Kampuni ya udalali wa bima ya Busara.

Wamfungua shauri hilo dhidi ya Dk. Martha ambaye ni mfanyakazi wa MDH pamoja na msimaizi wa mirathi ya Tarsila, Justine Edwald (kaka wa marehemu).

Jaji Mwanga alitoa ushauri huo juzi kwa shirika hilo na kampuni hiyo ya bima baada ya kupitia maelezo ya awali ya kesi hiyo pamoja na kusikiliza hoja (mabishano) ya pande zote kama shauri hilo ni la kuingiliana (interpleader suit). 

"Ninaashauri, kesi hii ina tuhuma kubwa za kughushi, kwa maana hiyo ni vyema kufungua kesi ya jinai ya kughushi," alisema Jaji Mwanga.

Katika shauri hilo, Dk. Martha kupitia mawakili wake, Water Chipeta na Saimon Lyimo, amejibu maombi yaliyowasilishwa na wadai hao kwamba anastahili kulipwa asilimia 40 ya bima ya maisha ya marehemu Tarasila.

Pia anadai kwamba kesi iliyoko mahakamani imekosewa, hivyo ameweka mapingamizi mawili ya awali ambayo yatasikilizwa Agosti 22, 2024 mbele ya Jaji Mwanga.

Katika mapingamizi hayo, Dk. Martha anadai kuwa kesi hiyo haikupaswa kuletwa kwa 'interpleader suit', anaomba itupiliwe mbali na pia ni matumizi mabaya ya mahakama.

Shirika hilo limefungua madai dhidi ya Tsere na Edwald ili mahakama iamue nani anastahili kulipwa bima hiyo ya maisha na kwa kiwango gani. 

Katika fomu ya warithi ya Group Life Insurance, inadaiwa Dk. Martha anataka alipwe asilimia 40 ya kiwango cha fedha cha bima hiyo ambacho ni Sh. 478,557,322.00.

Upande wa dalali wa bima hiyo na MDH, unadai kupata wasiwasi "inakuaje mtu asiye ndugu kupewa kiwango hicho cha fedha bila ushahidi wowote?" Hivyo, ukahitaji uthibitisho zaidi kama kweli marehemu aliandaa fomu hiyo au la. 

Katika fomu hiyo ya madai, inadaiwa kuwa uongozi wa MDH uliamua kushirikisha Jeshi la Polisi Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi (Forensic Bureau). 

Inadaiwa kitengo hicho kilibaini mwandiko na saini katika fomu hiyo si za marehemu Tarsila Oisso, aliyekuwa mfanyakazi wa shirika hilo.

Kutokana  na matokeo hayo, Inadaiwa MDH ilipeleka shauri Mahakama Kuu ili chombo hicho kiamue usahihi wa fomu na uhalali wake.  

Inadaiwa katika fomu hiyo ya madai kwamba, uchunguzi wa kitengo hicho cha Jeshi la Polisi, ulibaini fomu hiyo ilighushiwa Disemba 16, 2022, jambo linalodaiwa kumsukuma mwajiri kuamua kufungua shauri la kuingiliana (interpleader suit). 

MDH pamoja na dalali wa bima hiyo walifungua shauri hilo dhidi ya Dk. Martha na Edwald ili mahakama iamue nani anastahili kulipwa bima hiyo ya maisha na kwa kiwango gani. Mfamasia huyo (Tarsila) alifariki dunia Disemba 21, 2022.  

Katika fomu hiyo ya madai iliyoko mahakamani, inadaiwa kuwa fomu ya mgawanyo wa bima ya maisha ya Tarsila ilighushiwa wakati ambao mfamasia huyo alikuwa katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU) cha moja ya hospitali kubwa jijini Dar es Salaam ambako alikuwa anapata matibabu ya maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.