Dereva alivyoponyoka vitani Goma, mkewe nchini afa kwa hofu

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:39 AM Feb 14 2025
Said Idd Said.
Picha: Restuta James
Said Idd Said.

DEREVA aliyekwama siku tatu Goma, nchini Congo amesimulia alivyoishi maisha magumu aliyopitia mjini humo hadi kumpoteza mke wake kwa mshituko wa vita hivyo.

Ni Said Idd Said, mkazi wa Kivule, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam. Wakati vita inalipuka mjini Goma hadi waasi wa M23 kuuteka uwanja wa ndege wa mji huo, mwishoni mwa Januari, Said alikuwa ndio ameingia Goma kushusha mafuta ya petroli, uwanjani hapo.

Akisimulia mkasa huo kwa majonzi na gazeti hili jana, Said baba wa watoto watano akiwamo mdogo wa miaka miwili, amesema vita hivyo, vimeacha doa kubwa kwenye maisha yake hasa baada ya kumpoteza mke wake kipenzi, Asha Majid Liamzito (35).

Amesema aliondoka Tanzania Januari 16 kuelekea Goma, safari ambayo kwa kawaida humchukua siku nne hadi tano, lakini wakati huu iliwachukua siku tisa kuingia mji huo.

Alianza kuhisi hali isiyokuwa ya kawaida alipovuka mpaka wa Gisenyi (Rwanda) kuingia Goma, kwa kuwa jamaa zao wanaoishi Goma walionekana kuwa na wasiwasi huku wakiwaambia muda wowote, waasi wa M23 watauteka mji huo.

Maelezo hayo yalipewa nguvu na uamuzi wa shule kuwarejesha nyumbani wanafunzi, waliotangaziwa kwamba hali sio nzuri hivyo wasiende shule.

Alilazimika kumpigia jamaa yake mmoja ambaye alimhakikishia kwamba mji huo upo kwenye hatari ya kumilikiwa na waasi hao.

“Nikampigia meneja wa kampuni yetu Congo na nikampigia pia bosi wangu. Wakaniambia nisiwe na wasiwasi. Kwa kuwa tulikuwa tumevuka Rwanda, zikaanza taratibu za kuingia Congo, yaani kupata nyaraka za kuingia,” anasema.

Anasema walikaa hapo siku nzima na kesho yake, alikuwa meneja wao kampuni anayoifanyia kazi ambaye aliwaambia kwamba anaharakisha mchakato wao ili waende kushusha mafuta haraka na kugeuza kurudi Tanzania.

Siku hiyo hiyo, walifanikiwa kupata nyaraka na kuruhusiwa kuendelea na safari.

“Lakini tulipita njia ambayo huwa hatupiti. Tukaenda hadi uwanja wa ndege ambako ndipo tulipaswa kushusha mafuta,” anasema.

Said anasema siku ya tisa yaani Januari 25, 2025 ndipo walifanikiwa kuingia uwanjani hapo.

MILIO YA RISASI

Anasema waliingia eneo hilo majira ya saa sita mchana, wakisikia milio ya risasi mfululizo mchana kutwa, hali iliyowafanya waishi kwa wasiwasi kutokana na milio hiyo kusogea karibu kadiri muda ulivyokwenda.

Anasema madereva wawili walifanikiwa kushusha mafuta na kutakiwa kuondoka, waliokuwa bado wakalazimika kusubiri kuendelea na kazi hiyo kesho yake.

Anasema kulivyopambazuka, iliendelea milio ya risasi kiasi cha kushindwa kushusha mafuta na kutafuta namna ya kujinusuru ili wasipoteze maisha.

“Wakati wote nilikuwa nawasiliana na familia yangu, mke wangu na watoto pamoja na ndugu zangu wengine. Kuna wakati tuliongea akawa anasikia kabisa milio ya risasi, nikamwambia mtuombee,” anasema.

Anasema siku ya pili wakiwa uwanjani hapo, waasi waliuteka uwanja huo, na kwamba walikuwa wamesalia madereva wanne kushusha mafuta.

Said anasema wakati waasi wakizidi kusonga mbele, wao walifanikiwa kuokolewa na wanajeshi wa Afrika Kusini, ambao waliwaingiza kwenye kambi yao.

Anasema walilindwa na wanajeshi wa Afrika Kusini, ambao walikuwa wanapiga risasi kuwatisha waasi.

“Baadaye hali ilikuwa mbaya, wanajeshi wakaingia kwenye geti nyingine hapo hapo uwanjani. Tukapewa maelekezo ya kuchuchumaa. Tulikuwa Watanzania wanne na watu wengine kama saba, ambao wanajeshi walituvusha kutupeleka uwanjani kwenye zile njia za ndege kuruka,” anasema.

Anasema uwanjani hapo, walipewa maelekezo ya kuingia kwenye kontena fulani linalotumika kama ofisi pale.

“Hapo kila mtu alisali kwa lugha anayoijua kwa sababu tulishuhudia namna M23 walivyokuwa wanapiga risasi hadi wanaingia uwanjani. Nilimtaarifu mke wangu na nikamwambia nazima simu kwa sababu tuliambiwa tufanye hivyo.” 

Hapo palikuwa ni eneo hatarishi zaidi kwao, kwa kuwa risasi za waasi zilipigwa kuelekezwa eneo hilo na waliona waziwazi namna risasi zilivyokuwa zinapigwa.

“Niliangalia namna walivyokuwa wanapiga risasi kwa muda kama wa dakika mbili hivi. Walikuwa wanapiga mfululizo, kisha wanarudi nyuma wanakuja wengine wanapiga tena risasi mfululizo. Walikuwa ni kama wanabadilishana hivi…kwa kweli hali ilikuwa ya kutisha mno.” 

Mapigano hayo yalidumu kwa takribani saa mbili na waasi wakaingia rasmi uwanjani hapo na kuuteka.

Anasema bila kujua, hali ya Goma ilimpa wasiwasi mkewe ambaye muda wote alitamani wawe wanazungumza ili kujua usalama wa mumewe.

“Hali ilivyotulia, niliwasha simu na kumpigia tena mke wangu, lakini saa chache baadaye mawasiliano ya simu kwenye eneo hilo yalikatwa.”

Anasema anaamini mke wake alimtafuta bila mafanikio, jambo lililomfanya apate mshtuko na kuanguka ghafla akiwa nyumbani kwake Kivule.

Mkewe alipelekwa hospitali ya jirani, ambayo alipewa huduma na kuhamishiwa Amana, ambao nao walimpeleka Mloganzila.

Januari 30, asubuhi, alikumbuka kuweka kwenye simu yake line ya simu ya Rwanda, ambayo ilimpa mawasiliano na nyumbani. Siku hiyo, ndio walifanikiwa kuondoka Goma kuvuka kueleka Rwanda.

Anasema alipopiga simu ya mke wake, alipokea ndugu yake ambaye alimwambia mkewe amepata shida kidogo na yuko hospitali amelazwa.

“Nikapiga video kuwaomba wanioneshe mke wangu, wakanionesha akiwa kitandani, lakini sikuweza kuongea naye,” anasema.

“Nilioneshwa tu kalala, sikumwona uso, nikaona amelala tu. Nikapata matumaini tu kwamba huenda amezidiwa tu,” anasema.

WALIVYOONDOKA GOMA

Waliondoka mji huo wakiacha magari hayo pamoja na mabegi yao, kwani walilazimika kuvaa majaketi na kubeba nyaraka muhimu kama hati ya kusafiria, leseni ya udereva na fedha kidogo walizokuwa nazo.

Anasema waliondoka kwa kupitia kichochoro wakiwa wameinama, baada ya kuelekezwa njia ambayo ingewafanya wakutane na usafiri wa bodaboda kuwapeleka mpakani Goma.

“Ni kama umbali wa kilometa nne kutoka tulikokuwa, lakini tulilipa Dola za Marekani 20 kwa boda na hata ingelazimu kulipa zaidi hatukuwa na namna. Tulifanikiwa kufika mpakani salama,” anasema.

Walipofika mpakani, walifanya mawasiliano na ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda, ambao uliwasaidia kwa kuwatumia gari hadi Kigali na ndio uliowasiliana na baadhi ya watu waliofanikisha Watanzania hao kuondoka Goma salama.

“Nilipovuka na kuingia Rwanda nikapokea simu kutoka kwa mtoto wa kaka yangu akinuuliza narudi kwa usafiri gani. Alipokata tu simu, nilipata mashaka makubwa sana,” anasema.

Anasema alilazimika kumpigia mama mkwe wake, ambaye alipokea na kuongea kwa huzuni ndipo ndugu akamnyang’anya simu na kumwambia mke wake amefariki.

“Kwa kweli sikutegemea kupokea ujumbe ule, katika mazingira yale. Ilikuwa taarifa mbaya sana, nikadondosha simu, nililia mno. Bahati nzuri hatukukaa muda mrefu, gari ya ubalozi ikawa imefika, kutuchukua.” 

Serikali kupitia ubalozi wake nchini Rwanda, uliwasaidia kwa kiasi kikubwa na kuona kama wapo nyumbani Tanzania.

*Itaendelea kesho