BINGWA wa Magonjwa ya Figo na Mfumo wa Mkojo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Jonathan Mngumi, amesema unywaji duni wa maji au uliopitiliza mahitaji mwilini, huathiri mfumo wa mkojo, figo na kibofu.
Amesema unywaji maji kwa siku hutakiwa kuwa wa wastani kulingana na kazi anayofanya mtu, lakini ni lazima kwanza mtu asikilize kiu yake na si vinginevyo.
Bingwa huyo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Figo MNH, ameyasema hayo katika mazungumzo na Nipashe kuhusu unywaji maji, akisema kiasi cha maji kwa mtu anayefanya kazi nzito hasa juani, anayetoka jasho jingi, ni kati ya lita tatu hadi tano kwa siku.
"Kwa wastani mtu mzima anayefanya kazi nzito juani au kazi ya kutoka jasho jingi anashauriwa kunywa maji kati ya lita tatu hadi tano kwa siku kulingana na kiwango cha jasho na unyevunyevu wa mazingira.
"Ishara za mwili, ikiwa mtu anajisikia kiu sana au mkojo wake ni wa rangi ya njano iliyokolea, ni dalili ya ukosefu wa maji mwilini na anapaswa kuongeza unywaji maji," anasema.
Mtaalamu huyo anasema unywaji maji usio sahihi kwenye viungo vya mwili, pia unywaji duni, huchangia kuathiri viungo kadhaa muhimu kama vile figo, ngozi, moyo na ubongo.
"Wastani wa kujisaidia haja ndogo kwa saa 12 mpaka 24 kwa mtu mwenye afya njema ni mara nne hadi saba kwa siku, ni kawaida sawa na kila baada ya saa tatu hadi nne.
"Kujisaidia haja ndogo kwa saa 12 ni mara mbili hadi nne ndani ya muda huo. Kwa saa 24 kujisaidia ni mara nne hadi saba, kulingana na kiwango cha unywaji maji na shughuli za mwili," anafafanua.
Bingwa huyo pia anaonya unywaji maji kwa kiwango kilichopitiliza, akiwa na maelezo kuwa kuna madhara iwapo mtu atakunywa maji mengi kwa muda mfupi kiasi kwamba mwili hauwezi kuyatoa au kuyasawazisha kwa njia ya mkojo.
"Kwa watu wengi wazima, kunywa zaidi ya lita tano za maji kwa siku au zaidi ya lita moja au lita moja nusu kwa saa kunaweza kuwa hatari," anaonya.
*USIKOSE MAKALA KUHUSU SUALA HILI KATIKA GAZETI HILI KESHOKUTWA, ALHAMISI
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED