Balozi Ruhinda afariki dunia

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 05:24 AM Jun 16 2024
Balozi wa zamani wa Tanzania katika nchi za Canada na Jamhuri ya Watu wa China na mhariri maarufu wa vyombo vya habari nchini, Ferdinand Ruhinda.
Picha:Maktaba
Balozi wa zamani wa Tanzania katika nchi za Canada na Jamhuri ya Watu wa China na mhariri maarufu wa vyombo vya habari nchini, Ferdinand Ruhinda.

BALOZI wa zamani wa Tanzania katika nchi za Canada na Jamhuri ya Watu wa China na mhariri maarufu wa vyombo vya habari nchini, Ferdinand Ruhinda amefariki dunia.

Taarifa iliyotolewa jana ilieleza kuwa mwanadiplomasia huyo, mwanahabari na mfanyabiashara, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Ruhinda ambaye aliwahi kuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo, na yale ya Serikali ya Daily News, Sunday News kwa nyakati tofauti, atazikwa kesho (Jumatatu)  katika makaburi ya Kondo, Kunduchi,  Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya kisukari na msiba uko nyumbani kwake Masaki jijini humo. Alikuwa mwanzilishi wa magazeti ya Mwananchi kabla ya kuchukuliwa na kundi la kampuni za Habari la Nation na Radio Uhuru (sasa Uhuru FM).

Balozi Ruhinda ambaye anatoka familia ya uchifu, alipata elimu yake ya uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kupata mafunzo ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi.

Kabla ya kuingia katika medani ya diplomasia mwanzoni mwa miaka ya 1980, aliwahi kuwa Mhariri Mkuu wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) - sasa TBC Taifa.

Alihudumu ubalozi wa Tanzania nchini Sweden baadaye akateuliwa Balozi wa Tanzania nchini Canada (1983-1988) na China (1989-1992) kabla ya kustaafu.