Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranqhe, amezindua mitambo maalum ya kukarabati barabara za mitaa 154 pamoja na malori mawili mapya, hatua ambayo ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya jiji hilo.
Akizungumza mbele ya wananchi wa Jiji la Arusha, Iranqhe alieleza kuwa kila kata itapokea kiasi cha shilingi milioni 4, kwa ajili ya manunuzi ya vifusi vya kujengea barabara hizo. Huu ni msaada wa fedha ambazo zimebaki kwenye bajeti ya shilingi bilioni 2 zilizokuwa zimetengwa awali kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya ujenzi wa barabara.
Katika hatua nyingine, Mstahiki Meya alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira na aliwasihi madiwani kuhakikisha wanashirikiana na wananchi katika ajenda ya upandaji wa miti, hasa katika maeneo yanayokumbwa na ukame. Aliendelea kutoa tahadhari kuhusu ongezeko kubwa la utupaji wa taka mitaani, hususan chupa za plastiki zinazozagaa kwenye mitaro na maeneo ya wazi. Alisema hali hii inadhuru sifa ya Mkoa wa Arusha kama Kitovu cha Utalii kwa Tanzania Bara.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alieleza kuwa mitambo hiyo itahakikisha barabara zote za mitaa 154 zinazohitaji kukarabatiwa zinapata huduma. Aliwashukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, kwa usimamizi bora na ufuatiliaji wa karibu, ambao umewezesha jiji la Arusha kunufaika na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED