Alalamikia sera mpya NHIF kusumbua wateja

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:13 AM Sep 03 2024
Kadi ya NHIF.
Picha: NHIF.
Kadi ya NHIF.

MFANYABIASHARA, Shadiya Mtunzi, ameushauri Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kufanya maboresho kwenye sera mpya ya bima ya mtoto ili kuondoa sintofahamu zinazojitokeza kwa wateja wake.

Shadiya aliambia Nipashe kuwa anakosa baadhi ya huduma kwa sasa kwa kuwa mfuko huo unamtambua kama mteja mpya wakati ana zaidi ya miaka 10. 

Alisema alipitia kadhia hiyo baada ya kumwingiza mtoto wake kwenye kifurushi chake na kupitia mabadiliko hayo mfuko unamtambua kama mnufaika mpya na si wa muda mrefu.

Hata hivyo, NHIF imetoa ufafanuzi na kusema kuwa utaratibu wa mwanachama anayehama kifurushi kuanza upya ni wa kawaida na unajulikana na kila mwanachama.

Kaimu Meneja Uhusiano wa NHIF, Grace Michael, alisema mwanachama anayehama kifurushi analazimika kuanza upya kwa sababu kila kifurushi kinahudumiwa na dirisha tofauti.

Awali, akitoa malalamiko hayo, Shadiya alisema alichukua uamuzi wa kumjumuisha mtoto wake katika kifurushi chake baada ya mfuko huo kuondoa kifurushi cha watoto cha kulipia 50,400 na kuwashauri wazazi wawakatie watoto wao kupitia shule au kuwaunganisha kwenye vifurushi vyao.

“Mimi ni mwanachama wa NHIF kwa zaidi ya miaka 10 nipo katika taasisi binafsi ninalipa kifurushi kikubwa kile cha timiza.

Alisema baada ya taarifa hiyo alikwenda katika ofisi zao kwa ajili ya kumwingiza mtoto wake kupitia kifurushi na kushauriwa kuwa asubiri mpaka kifurushi kiishe siku atakayokwenda kulipia upya ndipo atamwingiza mtoto wake.

Alisema siku ilipofika walimpa namba ya kulipia malipo yake na mwanawe kwa ajili ya kumwingiza katika kifurushi ambacho tayari alikuwa ni mwananchama kwa zaidi ya miaka 10.

Alisema baada ya hapo walimtengenezea kadi mpya ambayo inaonesha sio mwanachama wa zamani bali ni mpya.

Baada ya siku kadhaa, Shadya aliugua na alipokwenda hospitali kwa kutumia kadi yake akajibiwa kuwa hana sifa ya kupata huduma nyingi kwa sababu ni mwanachama mpya wakati yeye ni mwanachama wa siku nyingi.

Baada ya kupata majibu hayo alilazimika kurudi NHIF na kupewa majibu kuwa mabadiliko ya sheria ndio yaliyosababisha yote hayo, hali ilimwacha akiwa na maswali kwanini serikali ibadilishe sheria bila kujua madhara yake.

Akitoa mfano, alisema zamani alikuwa analipa Sh. 600,000 kwa mwaka akiwa peke yake sasa hivi analipia Sh. 800,000 na kwamba badala ya kuonekana wa thamani zaidi sasa anaonekana amepoteza sifa kabisa.

“Mwanachama ambaye nimekuwa ninaweka fedha zangu kila mwezi na mimi ni mfanyabiashara ninahifadhi fedha kwa ajili ya kulipia, leo baada ya miaka 10 ninakwenda kupata huduma ninaambiwa sina vigezo na mbaya zaidi hata watumishi walioko ofisini hawajui madhara yaliyopo.”

“Sasa NHIF inatusaidiaje? Au inatugandamiza? Kama inaanzisha sera mpya kwa nini isifanyiwe majaribio kwanza kuona kama ni nzuri au mbaya?” Alihoji. 

Shadiya alisema kwa sasa ni mgonjwa anahitaji matibabu, lakini NHIF wanataka kumtumia kama mfano akisisitiza lengo lake anataka wajue nini wanapaswa kufanya kwa ajili ya kuendeleza shirika.

Aidha, alishauri sera ibadilishwe au iangalie namna ya kumaliza changamoto hizo, akisisitiza kuwa inakandamiza mwanachama kwa sababu kumwingiza mtoto kunasababisha mtu afutiwe taarifa zake zote za nyuma.

Alisema hataki atatuliwe tatizo hilo binafsi bali anataka iwe kwa wote wanaosumbuliwa na changamoto hiyo au sera hiyo ifutwe iwe kama zamani.