ACT kutinga ofisini kwa waziri wasimamizi kutofungua ofisi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:09 AM Nov 04 2024
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu.
Picha:Mtandao
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu.

CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema kinapanga kumwandikia msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa orodha ya wagombea wote wa chama hicho walioshindwa kuchukua na kurejesha fomu kutokana na wasimamizi wa uchaguzi kutofungua ofisi.

Chama hicho kimedai kwamba baadhi ya wagombea wake walishindwa kurejesha fomu kutokana na kufanyiwa hujuma na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi huo kufunga ofisi licha ya kuwa ndani ya muda.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, Kamati ya Uongozi Taifa ya chama chake, imetoa maelekezo kwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho kuandika barua hiyo.

Alisema lengo la kuandika barua hiyo ni kutaka wagombea wote walioshindwa kurejesha fomu kwa sababu ya ofisi za wasimamizi wa uchaguzi kufungwa, warejeshwe kwenye orodha ya wagombea.

Pia alisema maelekezo mengine ya kamati kwa Katibu Mkuu wa Chama ni kutaka awasiliane na vyama vingine makini vya siasa na wadau wa demokrasia nchini, ili kuandaa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha umma kupiga kura ya "hapana" kwa wagombea wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wamebaki peke yao au watabakishwa peke yao katika maeneo yao wakati wa mchakato wa uchaguzi huo.

Dorothy alisema kamati hiyo pia imemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kuhakikisha hatua zilizobaki za uchaguzi huo zizingatie misingi ya haki kwa kufuata sheria na kanuni zinazoongoza uchaguzi.

Maeneo ambayo chama hicho kimemwomba Rais Samia aingilie kati ni kwenye uteuzi wa wagombea, upigaji kura, kuhesabu na wakati wa kutangaza matokeo.

"Kamati ya Uongozi Taifa ya ACT-Wazalendo imesikitishwa na mwenendo usioridhisha wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hasa kwenye uchukuaji na urejeshwaji fomu, ikiwamo baadhi ya wasimamizi kufunga ofisi, mfano Kondoa Vijijini, Newala, Tunduma na Ulyankulu.

"Kukataa kupokea fomu za wagombea na kukataa maelekezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ya kuvipa vyama uhuru wa kuchagua ngazi ya chini ya kudhamini wagombea, mfano, kijiji cha Wari Ndoo, kata ya Machame Kaskazini, wilayani Hai, na maeneo mbalimbali ya jimbo la Ruangwa," alidai Dorothy.

Alisema kuwa pia kuna baadhi ya wagombea wao wanadai kupigiwa simu na watu wakiwatishia waliorejesha fomu wajitoe kuwa wagombea na kwamba jambo hilo limejitokeza kijiji cha Miuta, Tandahimba na mtaa wa Kanenwa, kata ya Kishiri, Nyamagana, mkoani Mwanza.