Waziri Bashe aiagiza TFRA kutoa mwongozo bei za mbolea kwenye vituo

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:49 PM Sep 23 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akikagua maghala ya Mbolea Mkoani Ruvuma.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akikagua maghala ya Mbolea Mkoani Ruvuma.

WAZIRI wa Kilimo,Hussein Bashe, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea(TFRA), kutoa mwongozo wa bei za jumla na rejareja kwenye kila kituo kinachouza mbolea nchini.

Waziri Bashe ametoa kauli hiyo  baada ya kutembelea maghala mbalimbali ya uhifadhi na uuzaji wa mbolea yaliyopo Songea mjini jana.

Kadhalika, Waziri Bashe ametembelea ghala la Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) lililokarabatiwa kwa ajili ya kuhifadhi na kuuza mbolea za kupandia aina ya DAP na za kukuzia mazao aina ya UREA linalopatikana katika eneo la viwanda la Ruhuwiko, Songea mjini. 

"Ghala hili lina ukubwa wa square metre 5000, kwenye ekari 16 na lina uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 za mbolea, litatoa huduma katika Mkoa wa Ruvuma na Wilaya zake zote,"amesema Bashe.

Pia, Kwa nyakati tofauti, amezungumza na Wafanyabiashara kujadiliana nao mambo mbalimbali ikiwamo bei wanazouza kwa wakulima.

 “Nashauri mkae pamoja kuwa na uwiano wa bei ambayo haimuumizi mkulima na pia iwe bei yenye gharama za uhalisia,” amesema Bashe.  

Kuhusu viuatilifu, Waziri huyo ameielekeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kuhakikisha viuatilifu vinasambazwa nchini na kuimarisha mfumo wa kanzidata kuongeza taarifa ya muuzaji na mnunuaji na kuweka 'QR Code' kwenye kila chupa au bidhaa. 

Wafanyabiashara hao ambao wamekutana na Waziri Bashe kutoka mkoa huo wa Ruvuma ni wale wa mauzo ya mbolea na mazao mbalimbali yakiwamo mahindi. 

 Waziri huyo ameomba wafanyabiashara hao endapo watakuwa tayari, wajenge maghala ndani ya Mkoa wa Ruvuma, na kwamba Wizara itaingia nao mikataba kupitia Taasisi yake ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kukodi kwa ajili ya kuhifadhi nafaka hadi za miaka 10.