'Watanzania pandeni miti, tumieni Nishati safi kulinda mazingira'

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 04:01 PM Jul 17 2024
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamisi Hamza Khamis (wa pili kulia), akimkabidhi cheti cha kuunga mkono matumizi nishati safi, Naibu Katibu Mkuu Ofisi hiyo, Christina Mndeme (kushoto).
PICHA: MWANDISI WETU
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamisi Hamza Khamis (wa pili kulia), akimkabidhi cheti cha kuunga mkono matumizi nishati safi, Naibu Katibu Mkuu Ofisi hiyo, Christina Mndeme (kushoto).

WATANZANIA wamehimizwa kupanda miti, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kutumia Nishati safi ya kupikia.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, aliyasema hayo wakati akizindua tamasha la 'Samia Nishati Safi Festival'.

Khamis, akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alisema jamii imuunge mkono Rais Samia Suluhu Hassan, ili ifikapo 2032 Watanzania wote watumie nishati safi.

"Tumuunge mkono Rais Samia ifikapo 2032 Watanzania wote tutumie nishati safi, si mkaa wa kuni. Upandaji miti ufanyike siku ya kukumbuka tarehe yako ya kuzaliwa, si kutumia muda mwingi kukata keki," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Up skills Tanzania, Tina Masaburi, alisema wanaumgana serikali kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

"Rais anahimiza matumizi ya nishati safi kama gesi, umeme, mkaa mbadala. Serikali iongezwe kasi ya upatikanaji rahisi wa nishati safi na Bei nafuu," alisema Tina.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Masaburi, ambaya aliandaa tamasha hilo, alisema jamii ijikite katika kutumia nishati safi, kuepuka athari zitokanazo na kuni.