Shinyanga watakiwa kutumia vyandarua kwa usahihi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 10:45 AM Feb 09 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akigawa vyandarua vyenye dawa kwa wananchi ambavyo vimetolewa na serikali ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akigawa vyandarua vyenye dawa kwa wananchi ambavyo vimetolewa na serikali ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuendekeza imani potofu juu ya matumizi ya vyandarua.

Amesema  vyandarua hutolewa na serikali, ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria na kuvitumia kwa matumizi yasiyokusudiwa, ikiwamo kuvulia samaki, kuzungushia bustani na kufugia kuku. Ni kinyume cha matumizi.

Amebainisha hayo wakati akizundua kampeni ya ugawaji vyandarua ngazi ya Kaya, mara baada ya kumalizika kwa uandikishaji, hafla iliyofanyika katika Zahanati ya Olshinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na chama.

Shinyanga watakiwa kutumia vyandarua kwa usahihi
Amesema kwa mwananchi ambaye ataendekeza imani  potofu na kutumia vyandarua ambavyo vimetolewa na serikali bure, kwa matumizi ambayo siyo sahihi, atachukuliwa hatua kali pamoja na kurudisha fedha ya chandarua alichopewa.

“Watendaji wa vijiji, vitongoji na mitaa, msione haya kuwachukulia hatua watu ambao watatumia vyandarua hivi vya serikali kwa matumizi yasiyo sahihi na sisi pia tutafanya ufuatiliaji kaya kwa kaya,” amesema Macha.

“Vyandarua hivi ni salama vina dawa ya kuulia mbu, na havihusiani na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume, wala kugunguni, vitumieni, ili mjikinge na ugonjwa wa malaria,” ameongeza Macha.

Amewasihi pia wananchi, kwamba katika kukabiliana na ugonjwa huo, wafanye usafi wa mazingira katika maeneo yao, ili kuondoa mazalia ya mbu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akigawa vyandarua vyenye dawa kwa wananchi ambavyo vimetolewa na serikali ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile ametaja takwimu za kiwango cha malaria mkoani humo ni asilimia 16, huku kitaifa ni asilimia 8.1 na Mkoa huo upo nafasi ya 4 kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Peter Gitanya, amesisitiza wananchi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vya na kwamba waachane na imani potofu, ili ifikapo 2030 kusiwepo na ugonjwa wa Malaria hapa nchini.

Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji kutoka Bohari ya Kuu ya Dawa (MSD), Victor Sungusia, amesema katika Mkoa wa Shinyanga kuna vituo 600 na watasambaza vyandarua kwa wananchi milioni 1.5 kwa wale ambao walijiandikisha mchakato utakaochukua muda wa siku 10.