Waazimia kuwaua mbwa wanaozurura

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 10:13 AM Feb 10 2025
Waazimia kuwaua mbwa wanaozurura.
Picha: Mtandao
Waazimia kuwaua mbwa wanaozurura.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha limeagiza halmashauri hiyo kuwaua mbwa ambao hawana walezi ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na mbwa hao.

Wamefikia hatua hiyo baada ya kuwapo taarifa za idadi kubwa ya mbwa ambao hawajapata chanjo na wanaendelea kuzurura mitaani huku kila mwananchi akikwepa kuwa mmiliki wa mbwa hao.

Akizungumza katika kikao cha Baraza  la Madiwani kilichofanyika mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Erasto Makala alisema mbwa ambao hawana walezi wanatakiwa kuuawa kama tahadhari ya madhara ambayo yanaweza kutokea kwa wananchi.

Makala alisema hakuna sababu ya kuendelea kuona idadi kubwa ya mbwa wakizurura mtaani ilhali hawajachanjwa. Mbwa ambao hawana walezi ni hatari.

Awali akiwasilisha hoja kuhusiana na mbwa hao katika kikao hicho, Diwani Shomari Mwinishehe alisema taarifa ya Idara ya Mifugo imebainisha kuwatambua mbwa 4,338, lakini waliopata chanjo ni 312 tu, hali ambayo inaonesha kuwapo kwa kasi ndogo ya uchanjaji mbwa hao.

"Tunaelezwa chanjo iliyoagizwa ni 628, sasa hawa mbwa wengine zaidi ya 3,000 wakiachwa bila kuchanjwa, hapo madhara ambayo yatatokea kwa jamii ni makubwa. Mbaya zaidi kila ukiuliza mlezi wa mbwa hao mtaani, kila mtu anawakataa," alilalama Diwani Shomari.

Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Regina Bieda aliahidi kufanyia kazi agizo hilo kuepusha madhara kwa jamii.

Sambamba na jambo hilo, kikao hicho cha madiwani pia kilitoa maelekezo kwa Idara ya Elimu kuhakikisha walimu wanaopangiwa kuhamia halmashauri hiyo, wanapelekwa maeneo ya pembezeni badala ya kuwaacha mjini ambako hakuna upungufu.

Madiwani walisema upungufu wa walimu maeneo ya pembezeni ni moja ya sababu ya kuwa na ufaulu duni huku baadhi ya shule za mjini zikiendelea kung'ara kitaaluma.