Simba ina matumaini ubingwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:18 AM Feb 09 2025
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids

KLABU ya Simba pamoja na kushushwa hadi nafasi ya pili, bado ina matumaini ya kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara huku taarifa zikisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids, amekataa kwenda FAR Rabat ya Morocco, akiamua kubaki kwenye mitaa ya Msimbazi.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kutokuwa na wasiwasi baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Fountain Gate, Alhamisi iliyopita, badala yake waendelee kuipa sapoti timu yao kila inapokwenda kucheza, kwani ina ubora wa hali ya juu ambao unawapa matumaini ya kurejea tena kileleni hivi karibuni.

"Simba ndiyo timu bora kwa sasa nchini, ukiona inapata matokeo mabovu ujue imefanya makosa mengi ya kujidhuru yenyewe, ukiangalia mechi dhidi ya Yanga ambayo tumepoteza, na hizi sare zote mbili ni makosa yetu wenyewe.

Lakini huo ndiyo mpira, Jumanne tunakwenda kucheza mechi dhidi ya Prisons, wanachama na mashabiki wa Simba sasa tuangalie mechi ijayo tuachane na mchezo huu uliopita.

Tumeshuka, tupo namba mbili kwa sasa, kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kufanya ili kurejea kwenye uongozi, niwaambie kuwa wasishtuke, pengo ni la pointi moja tu, kwa ubora tulionao tuna uwezo wa kurejea kwenye uongozi, kwa hili, kazi ndiyo kwanza imeanza," alisema Ahmed.

Kuhusu winga wa timu hiyo, Ladack Chasambi ambaye amekuwa kwenye midomo ya mashabiki wa soka na wachambuzi kutokana na kitendo chake cha kujifunga kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate, aliwataka Wanasimba wote wawe na kijana huyo kwani zipo kampeni zinatengenezwa kutaka kumpoteza.

"Kuhusu Chasambi anatuhitaji zaidi sisi familia yake, hatuna budi kumuunga mkono na kumuweka sawa kisaikolojia, ikumbukwe kosa alilolifanya lina faida kubwa sana kwa wapinzani wetu, sasa hao wameanza kumdhihaki ili wazidi kumpoteza asiwe kwenye ubora wake, tukasirike lakini tusimchukie kijana wetu," alisema.

Wakati hayo yakiendelea, habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa kocha Fadlu amepiga chini ofa ya FAR Rabat, ambayo ilikuwa inamhitaji kwa udi na uvumba.

Vyanzo kutoka ndani ya Simba na vingine kutoka nje ya nchi, vinasema kuwa Fadlu amekataa ofa hiyo  kutokana na kuridhishwa na kila kitu ndani ya klabu ya Simba, kuanzia uongozi, wachezaji na mashabiki wake ambao wamemfanya kujiona kuwa na amani na furaha kwenye kibarua chake ndani ya Simba.

"Ushirikiano wake na viongozi, kukubalika kwake na viongozi, wachezaji na mashabiki, vimemfanya kukataa kuondoka kwa sababu ndani ya Simba kwa sasa ni kocha anayeheshimika sana, nadhani uliona hata Bungeni Dodoma hivi karibuni Wabunge walivyomshangilia kwa nguvu na kwa muda mrefu lilipotajwa jina lake, yeye na kikosi chake walipolitembelea," kilisema chanzo.

Kutokana na kukataa ofa hiyo, FAR Rabat sasa wamewageukia makocha wawili, Alexander Santos, aliyetimuliwa hivi karibuni na CS Sfaxien ya Tunisia baada ya kufanya vibaya kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa kwenye Kundi A, pamoja na Simba, au kocha wa zamani wa Wekundu hao wa Msimbazi, Abdelhak Benchikha.