JUKWAA la Kitaifa la Asasi za Kiraia la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kanda wa Jukwaa la Asasi za Kiraia, wametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano DRC kwa kuwa yanaathiri eneo zima la Nchi za Maziwa Makuu.
Mjumbe wa Jukwaa la Asasi za Kiraia Nchi za Maziwa Makuu, Kennedy Walusalo, amesema hayo leo, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumnza na waandishi wa habari na kwamba wanaunga mkono maazimio yaliyotolewa na mkutano wa pamoja wa Wakuu wa Nchi za EAC na SADC.
Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), walikutana mwishoni mwa wiki na kutangaza hatua 13, ili kumaliza mgogoro mashariki mwa DRC.
Akifafanua zaidi, Walusalo alisema asasi za kiraia, zilizokutana jijini humo, Februari 7 hadi 9, mwaka huu, zinaunga mkono maamuzi ya mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za EAC na SADC.
“Kuongezeka kwa hali ya ukosefu wa usalama katika DRC, uwapo wa mgogoro huu kama hautashughulikiwa kwa dharura, kuna hatari ya kuzidi kuwa mbaya zaidi na kuhatarisha utulivu wa kanda nzima.“Kutokana na tishio hili, wadau wa asasi za kiraia walisisitiza haja ya kuongeza juhudi za pamoja kudai suluhisho la kudumu na shirikishi,” alisema.
Alisema kwamba maazimio hayo ni pamoja na kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuondolewa kwa vikosi vya kigeni vilivyoingia katika ardhi ya DRC bila mwaliko.
Pia alisema asasi hizo, zinaunga mkono azimio la kurudisha amani katika DRC, kupatikana kwa haki kwa waathiriwa wa machafuko haya.
“Washiriki waliunga mkono uamuzi wa kuunganisha michakato ya Luanda na Nairobi, ili kuwezesha mazungumzo kati ya DRC na Rwanda, huku wakisisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano mara moja na kwa ufanisi,” alieleza.
Walusalo alisema kwamba, washiriki walisisitiza umuhimu wa mtazamo wa pamoja wa kanda, ili kuhakikisha kwamba kuna mwitikio wa pamoja na wa kina kuhusu changamoto za kiusalama, kibinadamu, na kisiasa zinazoikumba DRC na Kanda ya Maziwa Makuu kwa ujumla.
“Tunatoa shukrani kwa wakuu wa nchi kwa kuitisha kwa wakati muafaka mkutano huu maalum kuhusu hali ya usalama katika DRC.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED