UCHAGUZI MKUU 2025: Dk. Nchimbi aelekeza mambo manne kwa wanachama CCM

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:25 AM Feb 10 2025
 Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Picha: Mtandao
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ameelekeza mambo manne kwa wanachama wa chama hicho wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza juzi jijini hapa wakati wa kikao cha Kamati ya Utekelezaji wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho, Dk. Nchimbi alitaja mambo hayo ni CCM kuwa chama cha kueleza sera na si matusi.

Balozi Dk. Nchimbi alitaja mambo mengine ni kuwa chama cha kuheshimu binadamu wengine, kuongelea maendeleo yaliyofanywa na serikali na kutotumia lugha za kebehi.

"Sisi tuendelee kujipanga kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu. Hiki si chama cha matusi, lazima tuwape nafasi wananchi wachague wenye sera," alisema.

Katibu Mkuu huyo alisema chama hicho lazima kiwe cha mfano katika kuhakikisha kinaheshimu binadamu wengine, kuongelea sera zao na maendeleo huku akisisitiza hawawezi kuishiwa hoja.

"Mambo ambayo serikali imefanya ni ya kutosha na watanzania wanapenda kuona mtu anayetenda. Tuna kila kitu cha kuwaeleza watanzania, hatuna sababu ya kuwa na lugha ya kebehi, hatuna sababu ya kuwa na matusi, tuwaachie ambao hawana vya kusema ndiyo watukane," alisema.

Balozi Dk. Nchimbi alisema katika historia ya CCM na jumuiya zake zote, ndiyo mara ya kwanza ameona kamati ya utekelezaji ya wazazi imeanza kupasha kwa kishindo kuelekea Uchaguzi Mkuu.

"Haijapata kutokea. Wakati ninakuja, nilijua nimealikwa kushiriki kamati ya utekelezaji ya wazazi. Shamrashamra hizi sikujiandaa, mmenitia msukosuko.

"Ninawapongeza  wazazi, sasa mmeelewa kwa kuwa mnakwenda kwenye uchaguzi mmeanza kupasha kidogo kidogo," alisema Balozi Dk. Nchimbi ambaye pia ni Mgombea Mwenza wa Urais Mteule kupitia CCM.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhili Maganya, alimshukuru Balozi Dk. Nchimbi kwa kushiriki kikao hicho, akibainisha kuwa waliamua kumwalika ili awasikilize na kuwashauri.

"Tunajua wewe ni siyo mjumbe lakini ni mtendaji wa chama. Tukaona tukualike utusikilize na wewe utushauri kadri unakavyoona. Tunashukuru umetupa uzito jumuiya. Sasa umetengeneza historia kwa mara ya kwanza tumeanza kuketi na wewe, hii ndiyo kamati ya utekelezaji, chombo kinachofanya kazi kwa niaba ya Baraza Kuu, umekubali kuja tena, ulijibu ombi kwa barua," alisema.