Mikopo ya asilimia 10 yarejeshwa kivingine

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:58 AM Feb 10 2025
Fedha.
Picha: Mtandao
Fedha.

BAADA ya kuripotiwa kuwapo udanganyifu, wakiwamo wakopaji hewa, mikopo kwa makundi maalum inayotolewa na serikali kupitia halmashauri, maarufu mikopo ya asilimia 10, sasa itasimamiwa na benki.

Serikali kupitia Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeingia mkataba na Benki ya CRDB kusimamia utoaji mikopo hiyo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayolenga kuwainua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kupitia mpango huo, benki hiyo itasimamia mikopo katika halmashauri tano: Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Dodoma, Manispaa ya Kigoma, Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua kali viongozi wa mikoa na wilaya watakaobainika kuhusika katika utoaji mikopo kwa vikundi hewa.

"Fedha hizi ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, hivyo lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa. Wakuu wa mikoa na wilaya ambao wataruhusu kuwapo vikundi hewa, watawajibika moja kwa moja. Wananchi wanapaswa kuwa waaminifu kwa kurejesha mikopo yao ili mpango huu uwe endelevu," alionya Mchengerwa.

Aliongeza kuwa zaidi ya Sh. bilioni 234 zinatarajiwa kutolewa kwa wananchi kupitia njia mbili: mikopo inayosimamiwa na benki katika halmashauri 10 na mikopo iliyoboreshwa katika halmashauri 174 nyingine.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alieleza utayari wa kushirikiana na Benki ya CRDB kuhakikisha mpango huo unafanikiwa. Aliwataka wananchi wa Dodoma na maeneo mengine kunufaika na mikopo hiyo kwa kuwekeza katika miradi endelevu.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa alishukuru serikali kwa imani waliyoipa benki hiyo. 

Alieleza kuwa uzoefu wa benki yao na taasisi yake katika usimamizi wa fedha na uwezeshaji wananchi utasaidia kuboresha usimamizi wa mikopo hiyo.

"Mpango huu unaendana moja kwa moja na jitihada zetu kupitia programu ya IMBEJU inayolenga kuwainua wajasiriamali wadogo. Tutatoa elimu ya fedha, ushauri wa biashara na kuhakikisha mikopo inawafikia walengwa kwa uwazi na ufanisi," alisema.

Tully alisema benki yao inajivunia kuwa sehemu ya mpango huo muhimu unaolenga kuinua uchumi wa wananchi na kukuza ujumuishi wa kifedha nchini.