WAFANYABIASHARA wameshauri serikali kuwekeza katika kuzalisha wataalamu watakaolisaidia taifa kuelekea miaka 25 ijayo badala ya wahitimu ambao wengi hawakidhi vigezo katika soko la ajira.
Pia wameshauri kuwa katika nguzo za rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kuanzishwe rasmi elimu rasmi ya biashara kuanzia shule za msingi, ili wanafunzi wawe na uelewa wa kutosha na kwamba mitaala ya elimu kuzingatia hilo.
Mfanyabiashara Benson Mahenya, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Tume ya Mipango na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini, uliohusu kuhakiki rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Kuna uhaba mkubwa sana wa wataalamu nchini. Bahati mbaya nguvu kubwa imeelekezwa katika uzalishaji wa wahitimu ambao kwa kiasi kikubwa hawafiki kwenye soko la ajira. Nchi yetu bado inaingiza wataalamu kutoka nje kwa sababu haizalishi wa ndani kwa kiwango kinachostahili. Mifumo yetu ya elimu izalishe watu ambao ni wataalamu watakaosaidia taifa.
"Kuna haja ya kufundisha elimu ya biashara kuanzia chekechea hadi vyuoni ili kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala muhimu ya kibiashara. Hiyo itasaidia kuzalisha wataalamu wazuri watakaolisaidia taifa," alishauri Mahenya.
Pia alisisitiza kuwa katika rasimu ya Dira ya Maendeleo 2050, kuwe na kifungu maalumu kinachoonesha mabadiliko ya sheria ambazo ni za zamani na kuweka za kisasa zitakazoendana na mazingira ya ufanyaji biashara ya sasa.
Naye Mfanyabiashara Satbir Hanspaul alisema matumizi ya mifumo ya kidijiti na Akili Mnemba (AI) yameongezeka maradufu miongoni mwa kampuni, benki na wafanyabiashara hata ambao wako mbali na miji kitu ambacho hakikuwapo kwa miaka 25 iliyopita.
Alisema kwenye rasimu ya dira hawajaona jambo hilo likiangaliwa sana kwamba Watanzania tunatumiaje fursa ya AI, huku akishauri kuwa ni muhimu kukawa na kituo maalumu kitakachofundisha teknolojia hiyo, ikiwamo shuleni ili kuwafanya wanafunzi na Watanzania kwa ujumla kuwa na uelewa wa kutosha.
Pia alishauri kuwa ni muhimu Tanzania pia kujifunza mazuri yanayofanyika katika nchi zilizoendelea kwa kuwezesha Watanzania kuzitembelea nchi hizo kisha kuwarudisha kwa ajili ya kuliendeleza taifa.
"Sisi vijana wetu wengi wanatoka nje ya nchi, wakitoka hawarudi. Marafiki wenzangu shuleni tulikwenda nchi fulani, tulikuwa kama 20 lakini tulirudi wawili," alishauri Hanspaul.
Aidha, alipendekeza kuwa kwenye elimu, kuna umuhimu wa kuwa na mitaala yenye kujumuisha masomo ya uchumi na biashara kwa kiasi kikubwa kwa kuwa Watanzania wengi wamekuwa na tatizo la kushughulika na masuala ya fedha jambo ambalo alisema linalirudisha taifa nyuma.
Hussein Sufian, alisema iko haja ya kuboresha huduma zinazopatikana katika biashara binafsi kwa kuwa na miradi mikubwa ya kimkakati hasa katika uwezeshaji wa upatikanaji wa mikopo itakayotumika katika uzalishaji.
"Kuna upungufu mkubwa kwenye sekta ya kilimo, sehemu kubwa ya watu wanaofanya katika sekta hiyo hawana fursa ya kupata mikopo kwasababu watu hawana imani nayo ni changamoto kubwa. Wakulima wamesahauliwa licha ya kuwa kwenye mnyororo wa uongezaji thamani," alisema Sufian.
Naye Dk. Judith Mhina, alipendekeza kuwa serikali iweke dira ya maendeleo ya miaka 200 ijayo badala ya 25, akisema hiyo itasaidia kuwa na mfumo mzuri wa kutenga maeneo kwa kuzingatia ukubwa wa eneo la taifa ambayo yataonesha wapi pametengwa kwa ajili gani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED