Wachezaji 10 bora wa wakati wote EPL

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:35 AM Feb 10 2025
 Cristiano Ronaldo
Picha: Mtandao
Cristiano Ronaldo

TANGU ilipofanyiwa marekebisho mwaka 1992, Ligi Kuu England (EPL), imekuwa nyumbani kwa wanasoka bora na wakubwa wa wakati wote.

Kuanzia miaka ya mapema ya Ligi Kuu, magwiji kama Eric Cantona hadi washindi wa Ballon d'Or kama vile Cristiano Ronaldo na wababe wa kisasa kama vile Mohamed Salah, mashabiki wa soka wameshuhudia nyota wengi wakali.

Lakini ni nani mchezaji bora wa Ligi Kuu England wa wakati wote?

Naam, twende hatua kwa hatua katika makala haya hadi mwisho, ambayo yanakudadavulia kila kitu...

10. Eric Cantona

Klabu: Leeds United, Manchester United, Nafasi: Mshambuliaji

"Eric alipokuja, alikuwa masiha. Alitubadilisha," alisema kocha Sir Alex Ferguson alipoulizwa kuelezea mchango wa Eric Cantona kwa Manchester United.

Nukuu hiyo moja kutoka kwa kocha mkuu wa wakati wote inasema kila kitu ambacho mtu anahitaji kujua kuhusu jinsi Cantona alivyokuwa mzuri.

Kujiamini kwake - ambako mwanamume yeyote aliye tayari kuvaa kola kwenye jezi ya soka anahitaji kuwa nayo - na ustadi wa kushangaza mara kwa mara ulifungua njia kwa miongo miwili ya United ya kutawala Ligi Kuu England.

9. Dennis Bergkamp

Klabu: Arsenal, Nafasi: Mshambuliaji

David Platt aliinua mpira juu ya safu ya ulinzi ya Leicester City na kuelekea kwenye mguu wa kulia ulionyoshwa wa Dennis Bergkamp. Baada ya kugonga mpira kwa ustadi na kugusa kwa mguu wake, nyota huyo wa Uholanzi anatumia mguu wa kushoto kumchenga Matt Elliott kwa ustadi wake kabla ya kufumua shuti lililojaa kwenye kona ya juu ya wavu.

Ikiwa umewahi kuliona bao hili, utajua haswa kwa nini Bergkamp ni mmoja wa wachezaji kumi bora katika historia ya Ligi Kuu England.

8. Frank Lampard

Klabu: Chelsea, Manchester City, Nafasi: Kiungo wa kati

Wakati kumuangalia Dennis Bergkamp alipokuwa anacheza inakufanya ufurahie soka, basi kuna mwingine aliyekuwa bora zaidi kumtazama na huyo ni Frank Lampard.

Mfungaji bora wa muda wote wa Chelsea, Lampard ndiye kiungo aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu England (177), katika misimu kumi. Lampard pia anashika nafasi ya tano kwa wachezaji waliotoa asisti nyingi akiwa nazo 102.

Mabao hayo yote na pasi za mabao ziliisaidia Chelsea kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu England na yeye mwenyewe kutwaa tuzo moja ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA.

Namba hazidanganyi, Lampard alikuwa bora kabisa.

7. Roy Keane

Klabu: Nottingham Forest, Manchester United, Nafasi: Kiungo wa kati

Roy Keane alikuwa mtu mkorofi wakati wa kucheza. Hakika, alikuwa mkorofi - kama kadi zake saba nyekundu kwenye Ligi Kuu zinavyothibitisha - lakini si hivyo tu.

Akiwa kwenye kilele cha nguvu zake, Keane alikuwa mmoja wa wachezaji wa kati bora zaidi duniani.

Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Jamhuri ya Ireland alikuwa kichocheo kikuu cha ubora wa Manchester United wakati wote wa uchezaji wake, akiwaongoza 'Mashetani Wekundu' hao kutwaa mataji saba ya ligi wakati wa maisha yake ya soka.

6. Mohamed Salah

Klabu: Chelsea, Liverpool, Nafasi: Mshambuliaji

Inashangaza kwamba, licha ya kuwa bado yuko katika kiwango bora cha maisha yake, Mohamed Salah tayari amefanya vya kutosha kuzingatiwa mchezaji bora wa sita katika historia ya Ligi Kuu.

Lakini hivyo ndivyo mchezaji wa soka Salah alivyo wa ajabu.

Akiwa amechezea Chelsea, Salah alirejea kutoka Ligi Kuu Italia, Serie A, akizichezea Fiorentina na AS Roma, kama mchezaji tofauti kabisa wa soka. Mshambuliaji huyo alirejea akiwa kama mfungaji asiyezuilika na mwenye uwezo wa kushangaza wa kukata kutoka upande wa kulia na kuukunja mpira kwenye kona ya juu kushoto apendavyo.

Na ingawa hilo linaonekana kama kutia chumvi, 'Mfalme wa Misri' ana Viatu vitatu vya Dhahabu vya Ligi Kuu kwa jina lake ambalo linathibitisha hivyo.

Pamoja na kufunga mabao, Salah pia ameweza kuwaunganisha wachezaji wenzake mara kwa mara pia. Katika misimu yake sita kamili kwenye klabu amekuwa na wastani wa kuchangia mabao 34 kwa msimu.

5. Kevin De Bruyne

Klabu:L: Chelsea, Manchester City, Nafasi: Kiungo wa kati

Katika enzi ambayo haijasikika hapo awali kiasi cha fedha na kipaji kuja kwenye mchezo wa Kiingereza, inasema mengi kwamba Kevin De Bruyne ambaye amekuwa mwanasoka bora asiyepingika kwa kipindi kirefu kama hicho.

Nyota huyo wa Ubelgiji amekuwa mtu muhimu kwa Man City katika kipindi cha kubeba mataji mengi zaidi klabuni hapo, na kuwa mmoja kati ya wachezaji watatu waliowahi kushinda tuzo za Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA mfululizo huku klabu yake ikinyanyua mataji matano ya ligi Kuu. Mtarajie kushinda mataji mengine zaidi kabla ya kutundika daluga zake.

4. Alan Shearer

Klabu: Blackburn Rovers, Newcastle United, Nafasi: Fowadi

Kuna takwimu moja ambayo imefafanua urithi wa Alan Shearer; ndiye mfungaji bora wa muda wote katika historia ya Ligi Kuu England.

Mabao yake 260 akiwa na Blackburn Rovers na Newcastle United ndiyo yanafaa kukumbukwa kwa wakati huu, kama vile msimu ambao alifunga mabao 34 na kutoa pasi 13 za mabao na kumfanya mchezaji huyo wa zamani kutwaa ubingwa wa ligi.

3. Wayne Rooney

Klabu: Everton, Manchester United, Nafasi: Fowadi

Yanasemwa mengi kuhusu kipaji cha Wayne Rooney kwamba, baada ya kutundika daluga zake akiwa Man Utd na mfungaji bora wa muda wote wa England, kulikuwa na sauti ya "nini kingekuwa?" Kuhusu kazi yake.

Alipoingia uwanjani kwa bao zuri dhidi ya Arsenal, ilionekana wazi kuwa Rooney angekuwa mchezaji mzuri wa kizazi chake. Na, licha ya kutokiongoza 'kizazi cha dhahabu' cha England kwenye Kombe la Dunia kama alivyotarajiwa, mtu hawezi kukataa kwamba Rooney alikuwa mwenye kipaji cha kushangaza wakati wa uchezaji wake.

Rooney alikuwa kielelezo cha uthabiti wakati wake akitamba kwenye Ligi Kuu.

2. Cristiano Ronaldo

Klabu: Manchester United, Nafasi: Mshambuliaji

Ikiwa tungetengeneza orodha ya wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kucheza kwenye Ligi Kuu England, bila shaka Cristiano Ronaldo angekuwa juu ya orodha hiyo. Akiwa mfungaji bora wa mabao katika historia ya soka, Ronaldo anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora wa muda wote duniani.

Ingawa alipata hadhi hiyo kutokana na uchezaji wake wa kustaajabisha akiwa Real Madrid ambapo alishinda Ballons d'Or nne, Ronaldo pia alifanikiwa kutwaa tuzo hiyo akiwa na Manchester United.

Alifanya hivyo mwaka 2008, baada ya kupaa kutoka mwanasoka bora wa Ligi Kuu hadi mchezaji bora zaidi duniani. Wakati wa msimu wa 2007/08 - ambapo alifunga mabao 31.

1. Thierry Henry

Klabu: Arsenal, Nafasi: Mshambuliaji

Ronaldo ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kucheza katika Ligi Kuu England, lakini Thierry Henry ndiye mchezaji bora zaidi wa Ligi Kuu England wa wakati wote.

Ingawa Ronaldo alikuwa na kipaji bora kwa ujumla, mtu hawezi kujadili kwamba kwenye Ligi Kuu, Henry alikuwa bora zaidi.

Kumtazama Henry akiwapita mabeki matata na kufunga bao zuri wiki baada ya wiki mwanzoni mwa miaka ya 2000 lilikuwa jambo la kufana kwa mashabiki wengi wa soka. 

Henry alikuwa uthibitisho kwamba mambo yanayotajwa kuwa ya kichawi yanaweza kuwa ya kweli kwenye uwanja wa mpira.

Gwiji huyo wa Arsenal aliimarisha jina lake katika viunga vya Ligi Kuu kwa misimu mitano mfululizo ya mabao 20, Viatu vinne vya Dhahabu, Viatu viwili vya Dhahabu vya Ulaya na uwezo wa kuiongoza timu yake hadi msimu wa kushinda taji ambao haujawahi kushuhudiwa.

Alikuwa kwenye kikosi cha Arsenal ambacho kilishinda taji la Ligi Kuu bila kupoteza mchezo hata mmoja.