DIRISHA la uhamisho wa majira ya baridi ya 2025 limekuja na kutoweka, huku klabu zote barani Ulaya zikiboresha vikosi vyao ikiwa ni nusu msimu huu.
Usajili huo ulihusisha baadhi ya watu wenye majina makubwa katika mchezo huo, lakini wengine hawakuweza kufanikisha kuhama.
Hawa hapa ni wachezaji watano wakubwa waliokosa uhamisho wa majira ya baridi.
Christopher Nkunku
Kuonekana kwa Marc Guiu akitokea kwenye benchi la Chelsea mbele yake Jumatatu usiku dhidi ya West Ham United kulizungumza mengi kuhusu hali ya Christopher Nkunku huko Stamford Bridge.
Mfaransa huyo yuko nje ya mawazo ya kocha Enzo Maresca, lakini licha ya kuhitajiwa na Bayern Munich na Manchester United, bado yuko Magharibi mwa London baada ya bei ya Chelsea ya zaidi ya pauni milioni 60 kuwatia hofu wale waliomtaka.
Nkunku sasa ana miezi sita ya kulazimisha kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha Chelsea, kabla ya kuondoka majira ya joto.
Alejandro Garnacho
Ilionekana dhahiri kuwa Alejandro Garnacho hangekuwa mchezaji wa Manchester United wakati dirisha lilipofungwa.
Huku ripoti nyingi zikisisitiza uwezekano wa kupatikana kwake, Garnacho alitajwa kama mbadala wa Khvicha Kvaratskhelia kule Napoli, ambaye uhamisho wake wa pauni milioni 59 kwenda Paris Saint-Germain uliipa timu hiyo ya Serie A nafasi kubwa ya kufanya makubaliano. United walisimama kidete, wakitaka karibu pauni milioni 70 ili kukubali kumuuza.
Napoli walifanya vibaya na kuruhusu Chelsea kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho. The Blues wanapenda kutumia fedha nyingi kuliko wanavyopaswa kuwanunua mawinga na huyu alionekana kupata uwezekano zaidi wakati ripoti za mpango wa kubadilishana Nkunku zilipoibuka. Hata hivyo, dirisha limefungwa na wachezaji wote wawili wamebaki nyumbani.
Oleksandr Zinchenko
Atletico Madrid na Borussia Dortmund zote zilitaka kumpa Oleksandr Zinchenko nafasi ya kuondoka Arsenal mwezi huu.
Nafasi ya mchezaji huyo wa Kimataifa wa Ukraine chini ya kocha Mikel Arteta ilionekana kutoweka wakati Riccardo Calafiori alipojiunga majira ya joto, na kuibuka kwa kiungo wa kati wa akademi Myles Lewis-Skelly kama chaguo bora la beki wa kushoto kumemsukuma Zinchenko kutokuwa na nafasi.
Sasa ni chaguo la tatu kwenye nafasi hiyo, Zinchenko anaonekana kujiandaa kwa pambano kali la kuwania nafasi ya kucheza katika kipindi kilichosalia cha msimu, lakini angalau anabakia mbele ya Kieran Tierney ambaye hivi karibuni ataondoka.
Andreas Christensen
Wakati Barcelona wanahitaji fedha, unaweza kuhakikisha kuwa Andreas Christensen atahusishwa na kuondoka. Ndivyo ilivyokuwa mwezi uliopita huu wakati klabu hiyo ya LaLiga ilipokuwa ikijaribu kufadhili uhamisho wa mkopo wa Marcus Rashford.
Timu za Ligi Kuu England zilianza kujipanga - Manchester United na Newcastle United zote zilihusishwa - lakini hakuna kilichotokea na Christensen sasa anajikuta katika vita vikubwa vya kurudisha nafasi ya kuanza kwenye kikosi.
Kocha Hansi Flick amemfufua Inigo Martinez pamoja na kijana Pau Cubarsi, huku Ronald Araujo akionekana kuwa wa kwanza kwenye mstari wa kurejea kikosini na Christensen ni wa nne katika viwango.
Douglas Luiz
Douglas Luiz alikuwa mmoja wa viungo waliohitajika sana barani Ulaya alipoondoka Aston Villa majira ya joto. Juventus ilishinda kinyang'anyiro cha kuwania saini yake, ikitengana na zaidi ya pauni milioni 40 na kumgeuza Mbrazil huyo kuwa chaguo la kupokezana.
Akiwa na mechi tatu pekee za Serie A kwa jina lake msimu huu, Luiz alihusishwa sana na kurejea England. Manchester City walimtaka arudi kwa mkopo, kama Chelsea, na kulikuwa na uwezekano wa kuhusishwa na Man Utd mwishoni mwa dirisha, lakini hakuna kilichotokea.
Tarajia hii kuibuka tena msimu wa majira ya joto, wakati klabu zitakapokuwa na fedha nyingi na Juventus watakuwa na busara zaidi na mahitaji yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED