Wakulima wa tumbaku walalama kulazimisha kutia saini mikataba

By Neema Sawaka , Nipashe
Published at 10:56 AM Sep 17 2024
Wakulima wa tumbaku
Picha: Mtandao
Wakulima wa tumbaku

WAKULIMA wa tumbaku katika Mkoa wa Tumbaku Kahama wamedai kulazimishwa kuingia mikataba ya miaka mitatu na kampuni za ununuzi wa tumbaku na baadhi yao wamegoma kuridhia mikataba hiyo wakidai ni ya kinyonyaji.

Imeelezwa kuwa wakulima hao wanahofia kuendelea kunyanyaswa na kukandamizwa, ikiwamo kucheleweshewa malipo. 

Udadisi wa mwandishi wa habari hii umebaini kuwa wanaogoma kufunga mikataba hiyo, wanatishiwa kufutwa na vyama vyao vya msingi pamoja na kuondolewa madarakani kwa viongozi wao. 

Mwandishi pia amebaini mikataba iliyofungwa kati ya wakulima kampuni wanazozitaka wakulima, haitambuliwa hali kadhalika kunyimwa na pembejeo za kilimo zinazotolewa kwa ruzuku ya serikali. 

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Shilabela Balemi AMCOS 2018, Amos Masanja, alisema jana mjini hapa kuwa wakulima wamegoma   kufunga mikataba ya miaka mitatu ya kulazimishwa kuwa chini ya kampuni za ununuzi wa tumbaku. 

Alidai kampuni hizo zinapigiwa debe na viongozi na kuwaletea waraka na barua za mashinikizo ya kuridhia mikataba hiyo bila kutoa uhuru kwa wakulima wachague kampuni wanayotaka kufanya nayo biashara. 

"Chama cha Ushirika ni muungano wa watu waliojiunga pamoja kwa hiari kwa madhumuni ya kufanikisha mahitaji yao kwa kuanzisha na kumiliki chombo chao kidemokrasia na kuchangia mtaji unaohitajika kwa usawa na kukubali kuyakabili matatizo na kupata manufaa kutokana na shughuli zake ambazo wao hushiriki kikamilifu," alisema. 

Aliongeza kuwa serikali imefanya mambo mengi mazuri kuhakikisha inawainua wakulima na kuwawezesha kulima kilimo chenye tija kwa kuwapatia masoko kwa kuwaletea kampuni nyingi za ununuzi wa tumbaku ili kuleta ushindani miongoni mwa kampuni. 

Alisema kuwa kwa kufanya hivyo, serikali imetoa fursa kwa wakulima kufanya uchaguzi wa kampuni za kufanya nazo biashara. 

Hata hivyo, Masanja alisema jitihada hizo zinakwazwa na wanachokilalamikia - wanalazimishwa na kuchaguliwa kampuni za kufanya nazo kazi. 

"Suala la kuingia mikataba ya miaka  mitatu limekuja ghafla na kuwapo kampuni nyingi kufanyike kwa kujinadi kwa AMCOS na wakulima     na ziende na sheria za ushirika ambazo zinaelekeza mwanachama ndiye mwenye uamuzi wa kuchagua kampuni kwenye mikutano ya vyama. 

"Na tukifunga mikataba ya miaka mitatu na kampuni moja, kampuni zingine zitapata wapi vyama na hizo kampuni nyingi za ununuzi wa tumbaku zilikuja kwa ajili gani?  

"Wanataka kuturudisha nyuma, kampuni zilipokuwa chache na mkulima alikuwa anapangiwa kiasi cha kuzalisha. Suala hili halikuja kwenye mrengo wa kumnufaisha  mkulima," alilalama Masanja. 

Alirejea barua kutoka bodi ikielekeza kufunga mikataba ya miaka mitatu (2024/25, 2025/26 na 2026/27) na vyama vyote vya msingi kuendelea kufanya biashara na kampuni walizouzia tumbaku msimu uliopita. 

Alisema kuwa imeelekezwa kuwa kila chama kibaki na kampuni yake waliyonunua tumbaku msimu uliopita ili kampuni iweze kufanya uwekezaji mkubwa. 

Emanuel Maziku, mkulima na kiongozi wa Chama cha Msingi Kazana AMCOS cha wilayani Kahama alisema "zamani tulikuwa tunatia saini mikataba ya miaka mitatu, lakini tulikuwa tunaihuisha kila mwaka. Ilikuwa fursa ya pande zote mbili - kampuni na vyama kubaki kuendelea kuwekeza katika hicho chama na kutoa fursa kwa chama kuihama kampuni. Mikataba ya sasa haitoi mwanya huo. 

"Mikataba imekuwa shida, vyama vimekosa uhuru wa kufanya uamuzi wao kwa mujibu wa taratibu na sheria za ushirika. Umelima na kampuni imekunyanyasa, imekucheleweshea malipo mpaka unaingia msimu mwingine hujalipwa na umekubaliana malipo kufanyika kwa dola, kampuni inakubadilikia na kukulipa kwa shilingi, unalazimishwa kuendelea nayo." 

Dotto Shinji kutoka Chama cha Msingi Isungasabo, kijijini Kangeme, Kata ya Ulowa, alisema kumekuwa na ucheleweshwaji malipo ya wakulima unaofanywa na kampuni za ununuzi wa tumbaku kinyume cha sheria za ushirika. 

Alisema sheria inataka wakulima walipwe ndani ya siku 14 tangu kuuza tumbaku, lakini malipo yamekuwa yanacheleweshwa hata  kwa zaidi ya miezi.

Ofisa Kilimo Halmashauri ya Ushetu, Elibariki Ndau, alisema wanasimamia maelekezo ya wizara, hivyo ni lazima mkulima ahamasishwe kufunga mikataba hiyo. 

Kwa msimu wa kilimo 2023/24 kampuni sita zilinunua tumbaku kilo 10,316,466 kwa dola za Marekani milion 24,303,288.71 sawa na wastani wa dola 2.36 kwa kilo ambapo kampuni ya AOTTL ilinunua kilo 2,079,029 zenye thamani ya dola 4,448,953, ikinunua kwa wastani wa dola 2.14. 

JTI ilinunua kilo 1,322,769 zenye thamani ya dola 3,149,210.12, ikinunua kwa wastani wa dola 2.38; MKWAWA ilinunua kilo 4,297,062 zenye thamani ya dola 9,913,484, ikinunua kwa wastani wa dola 2.31; G4 AGRO ilinunua kilo 1,039,643  kwa thamani ya dola 2,668,173 sawa na wastani wa dola 2.57. 

MASTERMIND ilinunua kilo1,194.262.70 kwa thamani ya dola 3,181,907.65 sawa na wastani wa dola 2.65 na OBAMCO ilinunua kilo 383,701 zenye thamani ya dola 941,561 kwa wastani wa dola 2.45.