Wakala adaiwa kutoweka zaidi ya wiki, mama adai alikuwa akifuatilia madeni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:51 AM Sep 17 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, SACP Michael Njera.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, SACP Michael Njera.

MFANYABIASHARA wa uwakala wa fedha za mitandao ya simu, utunzaji na ukopeshaji mjini Tarime, Kevin Masige anadaiwa kutoweka kwa zaidi ya wiki moja, hali iliyozua taharuki ikihusishwa na vitendo vya utekaji.

Akisimulia kutoweka kwa kijana wake, Mama yake Mzazi, Emakulata Masige, Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya Tarime, alisema wameshatoa taarifa polisi na kwamba kijana wake aliwapigia simu mwishoni mwa wiki kisha akakata.

Alidai kuwa Jumatatu Septemba 9, mwaka huu, saa kumi jioni, kijana alifunga duka na kuondoka kwenda Buhemba, nje kidogo ya Mji wa Tarime akidai anakwenda kufuatilia madeni ya fedha za mikopo kwa wateja wake.

"Kijana wangu hakurejea nyumbani tangu siku hiyo. Tulimaliza siku mbili pasipo kumwona, tukaenda kutoa ripoti Kituo cha Polisi Tarime, tulijaribu mara kadhaa kumpigia simu bila mafanikio kisha kuwataarifu ndugu na marafiki zake, wakiwamo wateja wake ili kutoa taarifa watakapomwona," alisema Masige.

Alidai kuwa Ijumaa iliyopita, kijana wake alipigia simu dada yake anayeishi jijini Mwanza, Magreth Masige, akidai yuko salama na baada ya muda mfupi alikata simu hiyo.

"Tulijaribu kumwuliza binti yetu huyo aliyempa simu kutupigia kuwa 'yuko wapi huyo Kelvin?', alisema kuwa aliondoka baada ya kupiga

simu na hakujulikana tena aliko," alisema mama huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, SACP Michael Njera, alithibitisha kupokea kwa taarifa hizo na kuwa zilitolewa katika Kituo cha Polisi Tarime na wanaendelea kufuatilia suala hilo.

Alimtaka mfanyabiashara ajitokeze na kuongea na wazazi wake ili kuondoa taharuki kwa familia na jamii.