Wageni wadaiwa kusafirisha mchele nje ya nchi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 09:35 AM Apr 11 2024
Mchele.
Picha: Maktaba
Mchele.

BAADHI ya raia kutoka nchini Uganda wanaoingia nchini kwa vibali vya kusalimia ndugu zao, wamedaiwa kufanya biashara ya mchele kwa kupeleka nchini kwao kinyume cha sheria na taratibu hali inayosababisha bidhaa hiyo kuadimika wakati wa mavuno na wakulima kukosa chakula cha kutosha.

Madai hayo yaliibuliwa juzi na Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mchele, Kata ya Kagongwa Manispaa ya Kahama, Malando Dila, kwenye kikao kazi cha kubaini kero wanazokabiliana nazo kibiashara na kudai wananunua zao hilo moja kwa moja kutoka kwa mkulima shambani na kusafirisha kwenda nje.

Alisema, wafanyabiashara wengi kutoka nchi za jirani hususani Uganda wanaingia nchini na vibali vya kusalimia ndugu zao na muda mfupi wanaanza kununua mpunga kinyemela moja kwa moja kwa wakulima shambani badala ya kufuata sheria na taratibu za kibiashara.

Dila alisema, hali hiyo inasababisha wakulima kuuza mpunga wao kwa bei ya hasara ambayo haiendani na bei ya sokoni wakati huo na wanafanya hivyo kutokana na uelewa mdogo wa wakulima, huku wakiiomba serikali kuingilia kati na kuwadhibiti.

Katibu wa wafanyabiashara hao, Joseph Phabiani, alidai kuwa baadhi yao wanaingiza mchele wa Thailand kwa kutumia vibali wanavyopewa na serikali na kuuchanganya na mafuta ya elizeti ili kuubadilisha rangi na kisha kuufunga kwenye vifungashio vyenye nembo ya Tanzania na kwenda kuuza nje.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita akizungumza na Nipashe alithibitisha kuwapo kwa wafanyabiashara hao kutoka nchi jirani ambao wanawafadhili wakulima na kuwauzia baada ya mavuno hali inayosababisha kuuza kwa bei ya chini na kukosa chakula.

Kuhusu kuingizwa kwa mchele wa Thailand, Mhita alisema jumla ya wafanyabiashara watano wa ndani walikamatwa kwa kuchukua mchele huo na kuuchanganya na mafuta ya elizeti ili kuubadilisha rangi  ufanane na unaozalishwa nchini.