Wachimbaji wadogo walia kuporwa maeneo na wawekezaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:08 PM Apr 02 2024
Wachimbaji wadogo wa madini.
MAKTABA
Wachimbaji wadogo wa madini.

WACHIMBAJI wadogo wa madini katika mgodi wa makongolosi Kijiji cha Majimoto, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamelalamika kuporwa maeneo na wawekezaji pasipo kulipwa fidia stahiki.

Wachimbaji hao walitoa malalamiko hayo wakati wa kikao baina ya wanakijiji na Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Lango la Matumaini Tanzania.

Nyigana Musa ni mmoja kati ya wachimbaji wadogo wa kijiji hicho alisema alishangaa kuona watu wakitumia eneo lake la uchimbaji pasipo makubaliano yoyote na kuambiwa kuachia eneo bila kulipwa fidia.

Hivyo aliiomba serikali kuwatazama kwa jicho la tatu ili kutatua tatizo ilo.

Aidha, aliutupia mzigo uongozi wa Serikali ya Kijiji Kwa kutochukua hatua zozote katika kuwasaidia wachimbaji hao.

Alisema baadhi ya maeneo wamiliki wamelipwa na mengine kutokulipwa sambamba na kunyang'anywa ubia wa kumiliki maeneo baada ya mwekezaji mzawa kuweka ubia na wawekezaji wa kigeni.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Daud Charles alikiri uwepo wa malalamiko hayo na kusema baadhi ya wanachama hawajalipwa, huku baadhi yao wakiwa tayari wamelipwa.

Alisema lakini bado wanalalamika kutokulipwa jambo linalosababisha sintofahamu katika uongozi wa Kijiji, huku akidai baadhi ya wachimbaji kutokuwa waaminifu baada ya kulipwa . 

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Lango la Matumaini Tanzania, Jackson Magesa aliiomba serikali kulichukulia suala hilo katika uzito ili kuondoa matatizo yanayowakabili wachimbaji hao na kuweka hali ya amani baina uongozi wa kijiji na wachimbaji.

Ofisa Madini wa Mkoa wa Mara, Amini Msuya alisema tatizo hilo linafanyiwa kazi na ofisi ya madini kwa kushirikiana na taasisi zingine.