Vituo vya kujaza gesi magari kuongezwa

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 12:20 PM Oct 04 2024
news
Picha: Mtandao
Gari linalotumia mfumo wa gesi.

IDADI ya vituo vya kujaza gesi katika magari vinatarajiwa kuongezeka kutoka vitatu vya sasa hadi 13 mkoani Dar es Salaam ifikapo Juni mwakani.

Mkakati huo unalenga kumaliza mateso ya madereva wa magari na bajaji kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu pindi wanapohitaji kujaza nishati hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi na Mafuta wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert alitoa ufafanuzi huo jana jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na waandishi wa habari baada ya juzi kutokea foleni ndefu ya kujaza gesi katika vituo maalum vilivyoko jijini.

Alisema foleni iliyotokea katika vituo vya kujaza gesi vya Ubungo na Uwanja wa Ndege ilisababishwa na hitilafu ya umeme katika kituo cha kujaza gesi kilichoko eneo la Tazara jijini.

Ni hitilafu anayoitaja ilitokea usiku wa kuamkia juzi na ilidumu kwa saa 21; imeshatatuliwa na huduma zinaendelea kutolewa.

Alisema hitilafu hiyo ilitokea katika kituo cha Tazara ambacho hakina mfumo mbadala wa kujiendesha pindi kunapotokea tatizo la umeme.

Gilbert alisema Mkoa wa Dar es Salaam una vituo vitatu pekee vya kujazia gesi, hivyo kimojawapo kikipata hitilafu, kunakuwa na msongamano kwa vyombo vya moto katika vituo viwili vilivyobakia kunakosababishwa na kushindwa kuhimili idadi ya wahitaji.

Ofisa huyo wa TPDC alisema: "Lengo la serikali ni kuhakikisha watumiaji wa vyombo vya moto vinavyotumia gesi, wanapata huduma ya uhakika. Hivyo, ifikapo Juni mwakani, tunatarajia kuwa na vituo 13."

Alisema kuwa katika kutatua kero ya uhaba wa vituo vya kujaza gesi, serikali imeshatoa leseni kwa kampuni binafsi 40 ambazo zimeonesha nia ya kujenga vituo hivyo.

Mkurugenzi huyo alisema changamoto inayosababisha sekta binafsi kushindwa kujenga vituo vya kujaza gesi kwa wingi kama ilivyo vituo vya mafuta, ni gharama za ujenzi wa kituo.

Alisema ujenzi wa kituo kimoja cha kujaza gesi unagharimu kati ya Sh. bilioni 2.1 na Sh. bilioni 2.7 kulingana na ukubwa na mahitaji ya eneo wakati kituo cha mafuta ni Sh. milioni 400.

Ofisa huyo alisema kuwa sasa idadi ya magari yanayotumia mfumo wa gesi nchini ni zaidi ya 4,800, lakini uwezo wa vituo vya kujaza gesi ni kuhudumia magari 1,200 hadi 1,500 kwa siku.