VIJANA na wanawake wajasiriamali wakiwamo wenye mawazo ya biashara, wametangaziwa neema ya mikopo yenye masharti nafuu kwa riba ya asilimia tisa.
Dhamana ya mikopo hiyo inaweza kuwa mali zinazohamishika, wazo la biashara, akiba iliyopo benki na mzigo wa mali alizonazo mkopaji.
Mkurugenzi wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake nchini (TWCC), Mwajuma Hamza, ameyasema hayo leo baada ya kutia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na benki ya Mwanga Hakika, itakayotoa mikopo hiyo.
Mwajuma anasema benki hiyo imekuja na huduma itakayowanufaisha wanawake na vijana, kwa kuwa inatatua changamoto ya mitaji inayowakabili wajasiriamali hao.
“Huduma hii inatoa unafuu wa upatikanaji wa mitaji kwa wanawake. Tumeona ni bora tukaingia makubaliano ili tuimarishe uhusiano wetu na kuleta tija kwa wanawake wafanyabiashara ambao kwa namna moja au nyingine, masharti ya mikopo kwenye baadhi ya benki yanakwamisha kukuza biashara zao,” anasema.
Anasema masharti ya benki nyingi ambayo yanadai dhamana ya mali zisizohamishika na riba kubwa, imekuwa ni kikwazo kwa biashara changa na za wanawake.
“Kwa mkataba huu, wanawake na vijana wanapewa uhuru wa kuchagua kitu cha kuweka dhamana. Kwa wenye mali kama nyumba, watakopeshwa na wenye mali nyingine kama mzigo wa dukani au wazo zuri la biashara. Benki imekuwa rafiki kwa wanachama wetu,” anasema.
Mkuu wa Idara ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, katika benki hiyo, Mwinyimkuu Ngalima, anasema ili kufanikisha hilo, wameanzisha akaunti maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wanawake na vijana, kwa kuwapa mikopo yenye riba ya asilimia tisa.
Anasema wajasiriamali wanaoweza kunufaika na mikopo hiyo, ni wenye biashara ndogo kama mama lishe, bodaboda na wale wenye biashara za kati, zikihusisha kuagiza mizigo nje ya nchi.
Ngalima anasema watakaonufaika na huduma hizo, ni wanawake na vijana wote nchini, hata katika maeneo ambayo benki hiyo haijafika.
Anasema mkataba huo umejikita katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wanawake hivyo kuwapa uwezo wa kuendesha biashara zao kwa ufanisi.
Anasema wakopaji watapewa elimu ya fedha na masoko, ili kuwapa maarifa na ujuzi, unaowasaidia katika kukuza
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED