Urus Tanzania yawashauri wafugaji kutumia mbegu bora za mifugo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:39 PM May 30 2024
Mkuu wa  Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akisikiliza maelezo kutoka kwa meneja mauzo wa  kampuni ya Urus Tanzania Meshack Anacleth namna kampuni hiyo inavyoewesha upatikanaji na usambazi wa mbegu bora za ng’ombe wa Maziwa na nyama.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akisikiliza maelezo kutoka kwa meneja mauzo wa kampuni ya Urus Tanzania Meshack Anacleth namna kampuni hiyo inavyoewesha upatikanaji na usambazi wa mbegu bora za ng’ombe wa Maziwa na nyama.

Urus Tanzania, ambayo ni kampuni tanzu ya Urus Global, inayojishughulisha na usambazaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa na nyama duniani,imewashauri wafugaji wazawa kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na kuboreshwa ili kuongeza uzalishaji katika shughuli zao za ufugaji.

Akiongea katika Maonesho ya 27 ya Wiki ya Maziwa yanayoendelea jijini Mwanza, Meneja Mkazi wa Urus Tanzania, Edson Mfuru alisema mbegu za Wanyama zilizoboreshwa siyo tu zinaongeza uzalishaji bali pia zinaongeza tija, faida na uendelevu mzuri wa ufugaji.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Uboreshaji wa Sekta ya Mifugo 2022/23-2026/27,pamoja na mafanikio kadhaa ambayo sekta imeweza kuyapata katika miaka ya hivi karibuni, bado sekta inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na ufugaji kwa kutumia mbegu za kienyeji ambazo zina uzalishaji mdogo.

Meneja huyo wa Urus Tanzania alisema kuhama kutoka kwenye ufugaji wa kutumia mbegu za kienyeji na kwenda kwenye mbegu zilizoboreshwa kunaweza kubadilisha maisha ya wafugaji na sekta nzima ya ufugaji kwa haraka. 

Mratibu wa kampuni ya Urus Tanzania inayojishughulisha na usambazaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa na nyama Noel Bohela (kulia) akimfafanulia jambo mteja aliyetembelea katika banda la kampuni hiyo wakati wa Maonesho ya 27 ya wiki ya Maziwa yanayoendele jijini Mwanza.
“Uhimilishaji ambao unapelekea upatikanaji wa mbegu iliyoboreshwa kama Girolando husaidia kuongeza wingi wa maziwa au nyama na pia ng’ombe huyu ambaye ni chotara anakua kwa haraka hivyo kwenda sokoni mapema na kupunguza muda na rasilimali ambazo zingetumika kumuhudumia,” alieleza.

Meneja mkazi huyo alifafanua kuwa, mbegu zilizoboreshwa au chotara zina uwezo mkubwa wa kuhimili magonjwa na hivyo hupunguza gharama za matibabu nakuongeza kuwa pia hupunguza uwezekano wa vifo na hivyo kumfanya mfugaji kuwa na uhakika na kazi yake.

“Uhimilishaji ambao hupelekea kupatikana kwa ng’ombe chotara kama Girolando, hufanyika ili kubadilisha chakula kuwa misuli kwa ufanisi zaidi. Chakula kidogo huitajika kwa ajili ya kuzalisha kiasi kikubwa zaidi cha maziwa au nyama. Matumizi ya chakula kidogo kulisha ng’ombe husaidia kupunguza gharama za ulishaji ambazo huwa kubwa katika ufugaji,”

Wafanyakazi wa kampuni ya Urus Tanzania inayojishughulisha na usambazaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa na nyama Modesta Kaihula (wa kwanza kulia) na Anande Munisy (wa pili kulia) wakiwafafanulia jambo wateja waliotembelea banda la kampuni hiyo wakati wa Maonesho ya 27 ya wiki ya Maziwa yanayoendele jijini Mwanza.
Mfuru alisema kwa sasa Urus Tanzania inafanya kazi na wafugaji katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Iringa, Njombe, Mbeya na Kagera, ikiwapa elimu juu ya mbegu bora na pia kuwapatia mbegu zilizoboreshwa katika maeneo yao.

“Ingawa kwa sasa tunapatikana katika maeneo niliyoyataja, lengo letu ni kuwafikia wafugaji popote walipo hapa Tanzania. Madhumuni yetu ni kuhakikisha kila mfugaji anafikiwa popote pale alipo na kupatiwa huduma zitakazomsadia kuboresha ufugaji wake. 

Tunaendelea kujitanua na kuboresha huduma zetu ili kukidhi mahitaji ya wafugaji wote,” aliongeza.