TANI 3,500 za ufuta zilizokwama kuuzwa tangu Juni 6, mwaka huu kutokana na mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kushindwa kufanya kazi zimeuzwa mwishoni mwa wiki katika Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Pwani.
Tani hizo zimeuzwa katika uzinduzi wa mnada wa zao la ufuta wa msimu wa mavuno ya mwaka 2024/2025 uliofanyika mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Kibiti baada ya uzinduzi wa mnada huo, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU), Mantawela Hamisi, alisema ufuta huo umeuzwa Sh. 3,653.21 kwa kilo.
Mantawela alisema Juni 6 ilitokea tatizo la kimfumo katika soko la bidhaa Tanzania na kusababisha ufuta huo kushindwa kuuzwa kwa siku ilivyopangwa na baada ya taratibu kufanyika mnada ulifanyika Juni 8, mwaka huu.
Aliwataka wakulima na viongozi wa vyama vya msingi vya kilimo AMCOS mkoani humo kuzingatia usafi wa zao hilo kabla ya kupeleka kwenye maghala.
Mwenyekiti wa CORECU, Mussa Mng'elesa aliwakumbusha wakulima wanaposafirisha mazao kuhakikisha wana nyaraka muhimu zinazotakiwa.
Mng'elesa pia amevielekeza vyama vya msingi vinapopokea mazao ya wakulima viwaeleze siku yatakapouzwa kwa njia ya mnada, huku akiwahakikishia wakulima kwamba pamoja na kikwazo cha barabara ufuta katika maeneo yote utakusanywa na kuuzwa kwenye minada.
Siku mbili kabla ya kufanyika mnada huo baadhi ya wakulima waliohudhuria uzinduzi wa mnada walisema kama suala la mfumo wa TMX halijakaa vizuri ni vema wakaendelea kutumia masanduku ili minada iende kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanal Joseph Kolombo, akiwa katika mnada huo wa uzinduzi ambao haukufanikiwa kufanyika kwa mara ya kwanza, alisema serikali haiko tayari kusikia suala la mkulima kucheleweshewa fedha zake baada ya mnada na badala yake kila mhusika anatakiwa kufuata taratibu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED