TRA yasifu matumizi mazuri ya fedha ujenzi Bwawa la Julius Nyerere

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:05 PM Feb 17 2026
TRA yasifu matumizi mazuri ya fedha ujenzi Bwawa la Julius Nyerere

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesifu matumizi sahihi ya fedha za kodi za Watanzania katika utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere, kufuatia ziara ya kikazi iliyofanyika Februari 14, 2026. TRA imesema mradi huo ni kielelezo cha namna kodi zinavyoweza kuchochea maendeleo kwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.

Ziara hiyo imewahusisha viongozi pamoja na Maafisa Elimu na Mawasiliano kutoka vituo vyote vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nchini, wakiwa na lengo la kujifunza na kujionea jinsi mapato ya kodi yalivyowezesha utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati wa taifa.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo, amesema ilikuwa muhimu kwa taasisi hiyo kutembelea mradi huo kwa kuwa ndiyo yenye jukumu la kukusanya kodi, hivyo walitaka kushuhudia kwa vitendo namna fedha za wananchi zinavyotumika na matokeo yake katika maendeleo ya taifa.

Alieleza kuwa Bwawa la Julius Nyerere linaonesha dhahiri jinsi kodi zinavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi kupitia kuongezeka kwa umeme wa uhakika, hali inayochochea biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi, na hatimaye kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

“Mradi huu unatupa ushahidi kuwa kodi za wananchi zinapotumika ipasavyo, huleta matokeo makubwa yanayoonekana na kugusa moja kwa moja maisha ya jamii,” alisema Bw. Kayombo.

Kwa upande wao, Maafisa Elimu na Mawasiliano wa TRA wamesema ziara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu uwekezaji wa Serikali katika sekta ya nishati na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati.

Wameongeza kuwa wataendelea kuwaelimisha wananchi kuwa kodi wanazolipa zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere, ambalo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya umeme katika Gridi ya Taifa na linachangia takribani megawati 2,115.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kituo hicho, Kaimu Meneja Uendeshaji na Udhibiti wa Mifumo wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere, Mha. Elinainyi Kalalu, amesema ziara hiyo imekuwa na tija kwa kuwa imewapa maafisa wa TRA fursa ya kujionea namna fedha za wananchi zinavyotumika na kurejesha manufaa kwa jamii kupitia huduma bora ya umeme.

Amesisitiza kuwa kituo hicho kitaendelea kuzalisha umeme kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha huduma ya uhakika kwa wananchi, huku akihimiza TRA kuendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa kuwa ndizo zinazoziwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Kwa ujumla, ziara hiyo imeimarisha uelewa kwamba ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati ni msingi wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, hususan katika sekta ya nishati ya umeme kwa ustawi wa Taifa.