TPA kuongeza ufanisi katika bandari zake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:16 PM Oct 07 2024
TPA kuongeza ufanisi katika bandari zake
Picha: Mpigapicha Wetu
TPA kuongeza ufanisi katika bandari zake

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa amesema kuwa mamlaka hiyo imejipanga kufanya upanuzi wa bandari zake, ili kuweza kuendelea kutoa huduma shindani katika Soko la Afrika na Kimataifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja ambayo imeanza jana, Mbossa amesema kuwa mpaka sasa mamlaka hiyo  imejiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kiushindani kutokana na uwekezaji wake unaoendelea katika bandari mbalimbali hapa nchini, ikiwa ni pamoja na mpango wa kupanua na kujenga gati 10 katika Bandari ya Dar es salaam ili kuongeza ufanisi na tija katika bandari hiyo.

“Katika kuhakikisha wateja wetu wanaendelea kupata huduma bora na stahiki sisi kama mamlaka tumekuja na mpango wa kuongeza gati 10 katika Bandari ya Dar es Salaam,”

“Hii inaenda kupanua soko la biashara kwa watumiaji wa bandari yetu kwani ufanisi utakuwa ni mkubwa na utakidhi mahitaji ya wateja wetu”, amesema.

Ameongeza kusema, TPA imeendelea kuboresha miundombinu ya bandari zake  ambazo ni pamoja na Bandari ya Bagamoyo, Bandari ya Tanga, Mtwara, Mbamba Bay na bandari  zingine ambazo ziko chini ya mamlaka hiyo.

Amesema hayo yote yanafanyika ili kuhakikisha kuwa TPA inachochea uchumi wa Taifa kupitia Bandari zake kwa kushirikiana na wawekezaji waliopo.

“TPA tumejipanga kuufungua uchumi wa Taifa kwa kutumia bandari zetu na ndio maana tumeendelea kuboresha maeneo mengi ya bandari zetu ili ziweze kutoa huduma kwa wateja wetu wa ndani na nje ya nchi”

“Kwa kupitia uwekezaji ambao tumeufanya katika bandari zetu,  matunda yake tumeanza kuyaona ambapo hadi sasa kumekuwa na utofauti mkubwa wa katika huduma za bandari ukilinganisha na miaka kadhaa ya nyuma”

“Hii inatokana na juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta mageuzi makubwa ya kiutendaji katika bandari zetu ili kuchochea biashara zaidi na kukuza uchumi wa nchi yetun”amesema Bw. Mbossa

1
Amesema kuwa hadi kufikia sasa sekta ya uchukuzi inachangia zaidi ya asilimia 7.3 ya pato la Taifa ikiwa malengo yaliyopo ni kufikisha asilimia 15 .

“Ili kufikia malengo, TPA  tumeanza kuungana na makampuni makubwa ya meli duniani ili kuhakikisha bidhaa zinakuja kwa wingi na kwa bei rahisi ili kuwarahisishia na kutanua wigo wa kibiashara na mataifa ya jirani “ 

“Pamoja na maboresho ya bandari zetu, TPA imeendelea kuboresha mifumo ya malipo hasa katika mfumo wa kidijitali ambayo itamuwezesha mteja kulipia bidhaa au mzigo wake popote alipo badala ya kwenda ofisini.

Pia Mbossa aliwataka wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuendelea kutumia bandari za Tanzania katika kusafirisha mizigo yao kwani ufanisi uliopo kw asasa katika bandari hizo ni mkubwa ukilinganisha na awali.

Naye Mkuu wa shughuli za kampuni   ya  kampuni ya Tanzania East Africa Getway Terminal Limited (TEAGTL) Donald Tawala amesema kuwa Bandari imekuwa ikifanya maboresho katika maeneo tofauti tofauti,  hivyo wao kwa kushirikiana na TPA wameendelea kufanya mageuzi makubwa katika uboreshaji wa huduma wanazozitoa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa mifumo ya malipo, uboreshaji wa mifumo ya kupakia na kushusha mizigo katika meli , na lengo mageuzi hayo ni kuhakikisha ufanisi katika bandari unaongezeka na kuwa na tija.