TASHICO: Usafirishaji njia ya majini ni nafuu, salama

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 10:29 AM Dec 09 2024

Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Eric Hamiss.
Picha:Mtandao
Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Eric Hamiss.

MKURUGENZI wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Eric Hamiss, amesema kusafirisha bidhaa kwa njia za majini ni nafuu zaidi na salama kuliko njia nyingine, kutokana na urahisi uliopo na uwekezaji uliofanyika katika sekta hiyo.

Alibainisha hayo juzi wakati akiongea na Nipashe na kueleza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa kwenye ujenzi wa meli utaongeza biashara ya ndani na nchi jirani.

“Ujenzi wa meli za mizigo utawezesha Tanzania kuimarisha biashara na nchi jirani kama Uganda, Kenya, Zambia, Burundi, DRC na Malawi, jambo ambalo litapanua soko kwa bidhaa za ndani na kuleta fedha za kigeni,” alisema Hamissi.

Alisema kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Kampala (Uganda) kwa barabara ni kilometa 1,717 lakini kutoka Dar es Salaam hadi Kampala kupitia Ziwa Victoria ni kilomita 1,470.

“Vilevile mizigo inayokwenda Kalemie, DRC ni rahisi kupita Ziwa Tanganyika kuliko kupita njia ya barabara, aidha upite Tunduma kisha Zambia km 1,922 au upitie Burundi km 1,877 lakini kutoka Dar es Salaam kwenda Kalemie (DRC) kupitia Bandari ya Kigoma ni kilomita 1,375,” alisema.

Hamissi baada ya uhuru, shirika lilikuwa chini ya uangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini serikali iliendelea kutoa huduma ya usafiri kwa njia ya maji katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa kutumia meli tatu.

“Hata hivyo, serikali ilinunua meli mpya saba, ambako MSCL ilianzishwa chini ya Sheria ya Makampuni Sura 212, Desemba 8, 1997 kutoka Shirika la Reli (TRC), lakini rasmi MSCL ilianza kazi Agosti 1, 1999 ikiwa na meli 14 na boti moja,” alisema.

Aliongeza: “Mwaka 2018, serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa minne katika Ziwa Victoria na mwaka 2022, serikali iliielekeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kukabidhi meli tatu  za Mv. Mbeya II, Mv. Njombe na Mv. Ruvuma kwa MSCL ambazo hadi sasa meli hizo zinaendelea kutoa huduma katika Ziwa Nyasa,” alisema.

Alisema katika awamu ya kwanza ya miradi 2018/23 ilihusisha miradi minne mojawapo ikiwa ni ujenzi wa meli mpya ya Mv. Mwanza “Hapa Kazi Tu”, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria, pamoja na ujenzi wa chelezo.